.webp)
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameweka wazi kuwa operesheni za kukagua eneo la Kariakoo usiku na mchana ni mkakati endelevu wa kuhakikisha soko hilo linabaki kuwa kitovu cha biashara kinachofikika wakati wote.
Mpogolo amesisitiza kuwa kuachwa wazi kwa barabara zinazozunguka Soko Kuu la Kariakoo, hususan Barabara ya Msimbazi, si suala la hiari bali ni takwa la kisheria na kiuchumi linalolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza msongamano ambao kwa muda mrefu umekuwa kikwazo kwa ukuaji wa biashara katika eneo hilo.
Katika ziara ya usiku iliyojumuisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, ilibainika kuwa serikali imedhamiria kurejesha nidhamu ya matumizi ya miundombinu ili kutoathiri shughuli za kiuchumi.
Mpogolo amebainisha kuwa barabara kuu kama Msimbazi, Uhuru, na Lumumba ni mishipa muhimu ya usafiri jijini na hazitahusika katika mpango wowote wa upangaji wa wafanyabiashara wadogo, kwani zinatakiwa kubaki wazi muda wote ili kuruhusu mzunguko wa magari, ikiwemo mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amefafanua kuwa Kariakoo ni eneo nyeti ambalo katika mwaka wa fedha uliopita pekee, kupitia Kanda Namba 2 inayohusisha soko hilo, liliweza kuchangia takribani shilingi bilioni 54 katika mapato ya halmashauri.
Mabelya amesema kuwa lengo la serikali si kuwaharibia wafanyabiashara mitaji yao, bali ni kutengeneza mazingira yaliyopangwa vizuri ambayo yatamfanya kila mfanyabiashara na mteja kuwa na uhuru wa kufanya miamala yake katika mazingira yenye hadhi ya kimataifa.
Msisitizo huu wa serikali unakuja wakati kukiwa na malalamiko ya wadau wengi wa biashara kuhusu kuzibwa kwa njia za watembea kwa miguu na magari, jambo ambalo limekuwa likishusha mvuto wa soko hilo kwa wafanyabiashara wa nje.
Kupitia ushirikiano na viongozi wa wafanyabiashara, serikali inatafuta suluhu ya kudumu itakayoruhusu biashara kuendelea katika barabara za ndani zilizotengwa, huku barabara kuu zikibaki wazi ili kulinda taswira ya Kariakoo kama soko kiongozi katika ukanda huu wa Afrika.