` SGR BANDARINI DAR NI MAPINDUZI YA KASI, TIJA NA USHINDANI WA KIUCHUMI

SGR BANDARINI DAR NI MAPINDUZI YA KASI, TIJA NA USHINDANI WA KIUCHUMI

 

TANZANIA imeingia katika hatua nyingine ya kihistoria baada ya Serikali kutangaza kuanza kwa huduma ya treni ya kisasa (SGR) kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Dodoma. 

Hatua hii, iliyotangazwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, inatajwa kuwa ni mwarobaini wa msongamano wa mizigo bandarini na chachu ya ukuaji wa haraka wa uchumi wa viwanda na biashara nchini.

Kuanza kwa huduma hii kuna maana kubwa kwa mfuko wa Mtanzania wa kawaida kwani SGR ina uwezo wa kubeba hadi tani milioni 25 kwa mwaka, jambo ambalo litapunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa kwa kiasi kikubwa. 

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, asilimia 80 ya mizigo inayopita katika maeneo ya reli hiyo sasa itabebwa na treni. Hii inapunguza utegemezi wa malori ya masafa marefu, hivyo kupunguza gharama za uingizaji bidhaa (imports) na kupandisha thamani ya mazao yetu yanayokwenda nje (exports) kwa kuwa yatafika sokoni kwa gharama nafuu.

Kimkakati, Serikali inajipanga kuanzisha bandari kavu katika mikoa ya Morogoro, Dodoma, na Shinyanga. Huu ni mpango unaolenga kuifanya Tanzania kuwa "Lango Kuu" la biashara kwa nchi nane zisizo na bahari. 

Malori kutoka nchi jirani sasa yataishia Isaka au Morogoro kufuata mizigo iliyoletwa na SGR, hatua itakayookoa muda na kulinda barabara zetu dhidi ya uharibifu wa magari mazito. Hii inaongeza uaminifu wa Tanzania kimataifa na kuvutia wawekezaji wakubwa wanaotafuta mifumo ya kisasa ya usafirishaji (logistics).

Kwa maendeleo ya Taifa, SGR siyo tu njia ya usafiri, bali ni mhimili wa mnyororo wa thamani. Uwezo wa kuunganisha huduma na kuboresha mifumo ya uendeshaji unawezesha bidhaa kufika viwandani na sokoni bila kuchelewa. Hii inatengeneza ajira mpya, inachochea ukuaji wa miji mipya pembezoni mwa reli, na kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye ushindani mkubwa kiuchumi ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (SADC).


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464