
Wakati mataifa mengi duniani yakihangaika na mtikisiko wa bei ya nishati, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameziba masikio dhidi ya maneno ya kubeza na badala yake amepiga hatua nyingine ya kihistoria inayoiweka Tanzania katika ramani ya mataifa yenye nguvu ya kiuchumi.
Kupitia uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa matangi 15 ya kisasa ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Rais Samia ameamua rasmi kuitumia jiografia ya Tanzania kama silaha ya kiuchumi, akiigeuza Tanzania kuwa "ghala kuu" la nishati kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hatua hiyo ya kijasiri inalenga kuimarisha akiba ya kimkakati ya mafuta (Strategic Fuel Reserve), ambayo itakuwa ni kinga madhubuti dhidi ya misukosuko ya kimataifa na mabadiliko ya bei katika soko la dunia yaliyopanda kwa 13% hivi karibuni.
Rais Samia ameweka wazi kuwa Tanzania siyo tu nchi ya kupitisha mizigo, bali ni kitovu (Hub) cha biashara kinachokusudia kuhudumia nchi nane zisizo na bahari kwa uhakika na tija. Maagizo yake ya kutaka mifumo ya TRA na TPA isomane ili kulinda kila senti ya mapato, ni salamu tosha kwa wote waliokuwa wakitegemea mianya ya ufujaji ili kuona Taifa likikwama.
Maboresho hayo makubwa, yanayoiwezesha bandari yetu kupokea meli kubwa aina ya Panamax, tayari yameanza kuleta matunda ya kishindo baada ya mapato ya forodha kupaa hadi kufikia Sh trilioni 12.31 kwa mwaka 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la karibu mara mbili kutoka Sh trilioni 7.3 za hapo awali.
Mafanikio haya yaliyopatikana kupitia uwekezaji makini wa kampuni ya DP World, ni jibu la vitendo kwa wakosoaji, yakionyesha kuwa Tanzania sasa imeamua kupaa kuelekea Dira ya 2050 bila kurudi nyuma. Hakika, kwa mkakati huu wa kuhakikisha usalama wa nishati na kuimarisha miundombinu, Tanzania inajipambanua kama taifa ambalo halitabiriwi tena, bali linaongoza njia.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464