` SERIKALI YAMPIGA MSASA KIJANA: WANUFAIKA WA UANAGENZI WAGOTA 93,495 NCHINI

SERIKALI YAMPIGA MSASA KIJANA: WANUFAIKA WA UANAGENZI WAGOTA 93,495 NCHINI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, ambapo hadi kufikia Februari 2026, jumla ya vijana 93,495 wamefaidika na programu za mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi.

 Mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga nguvukazi shindani inayokwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Awamu ya Nane ya mafunzo hayo katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Don Bosco jijini Dodoma, Machi 03, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, amesema kuwa serikali itaendelea kuimarisha sera na miongozo ili kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu. 

Waziri Sangu amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni daraja muhimu linaloziba pengo la ujuzi kati ya nadharia za darasani na vitendo vya kazini, hatua inayomsaidia kijana kuwa na uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe kwa tija.

Katika awamu hii ya nane (2025/26), jumla ya vijana 5,746 wamedahiliwa katika vyuo 46 nchini kote, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. 

Serikali imebainisha kuwa Tanzania inahitaji nguvukazi yenye weledi na uwezo wa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa. 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameipongeza serikali kwa kutenga bajeti maalum, akibainisha kuwa uwekezaji huo ni kielelezo cha thamani inayopewa rasilimali watu, hususani vijana ambao ndio nguzo ya uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Zuhura Yunus, ameeleza kuwa tangu kuanza kwa programu hiyo mwaka 2016/17, lengo kuu limekuwa ni kuongeza uzalishaji na ubora wa huduma nchini. 

Hata hivyo, wadau wa elimu wametoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuwawezesha wahitimu kwa vifaa vya kazi (startup toolkits) baada ya kuhitimu. 

Mkuu wa Chuo cha Don Bosco, Mhandisi Dkt. Justine Mulebya, ameshauri kuwa msaada wa vitendea kazi utawasaidia vijana hao kuanzisha karakana zao na hivyo kuwa waajiri wa vijana wengine badala ya kusubiri ajira rasmi. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464