` TAKUKURU SHINYANGA YADHIBITI MIANYA UPOTEVU MAPATO SEKTA YA AFYA USHETU

TAKUKURU SHINYANGA YADHIBITI MIANYA UPOTEVU MAPATO SEKTA YA AFYA USHETU

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kudhibiti upotevu wa mapato uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Hatua hiyo imeongeza makusanyo ya mapato kutoka Sh. milioni 3 kwa mwezi hadi kufikia Sh milioni 14, baada ya watumishi kupewa elimu kuhusu maadili, uwajibikaji na madhara ya rushwa.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy, amebainisha hayo leo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 kwa waandishi wa habari.
Amesema, kabla ya utoaji wa elimu hiyo kulikuwa na malalamiko ya upotevu wa mapato na huduma zisizoridhisha kwa wananchi katika vituo vya afya vya halmashauri ya ushetu.

“Baada ya kuwapatia elimu sahihi watumishi wa afya kuhusu maadili na uadilifu, tumefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema Kessy.
Ameongeza kuwa mbali na kudhibiti upotevu huo, huduma za afya zimeimarika katika vituo vyote vya kutolea huduma, huku wananchi wakipata huduma kwa haki na kwa wakati.

Katika hatua nyingine, taasisi hiyo imefanikiwa pia kudhibiti ukwepaji wa ushuru wa mazao katika halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kwa kuimarisha doria kwenye maeneo ya ukusanyaji ushuru, ambako awali kulikuwa na mianya ya upotevu kupitia njia zisizo rasmi.
Aidha, amesema wamefuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika shule ya msingi Magongwa, halmashauri ya Msalala, na kuokoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya sh milioni 51.7 ambavyo mzabuni alikuwa amenunua bila kuviwasilisha katika eneo la mradi.

Ametaja mikakati ya taasisi hiyo, ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya rushwa, kufanya uchambuzi wa mifumo ya utendaji katika taasisi za umma na binafsi, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma hasa kwenye miradi ya maendeleo.

Ametoa wito pia, kwa taasisi za umma kuzingatia misingi ya maadili katika utoaji wa huduma, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa bure kupitia simu 113.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464