Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Vijana kote nchini na nchi za jirani, wametakiwa kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi zinazotolewa na chuo cha VETA Shinyanga, ili kujiongezea uwezo wa kuajirika na kujiajiri, sambamba na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Abraham Mbughuni.
Wito huo umetolewa leo Marchi 2,026 na Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Abraham Mbughuni, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jitihada za chuo hicho katika kupanua fursa za ujuzi kwa vijana, kwa kuunga mkono maono ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amesema, VETA ni wakala wa Serikali ulioanzishwa kwa Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Sura ya 82, wenye jukumu la kuratibu, kugharamia na kutoa mafunzo ya ufundi stadi nchini, huku lengo kuu likiwa ni kuzalisha mafundi stadi mahiri na wa kutosha kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Veta ndiyo inazalisha watu wanaojenga tanzania kwa vitendo kwa kujenga nyumba tunazoishi, ujenzi miundombinu ya barabara, umeme, utengezaji wa mashine, huduma za utalii, tekonolijia za kilimo matengezo ya magari, vyote hivi vinatengemea mafundi kutoka VETA, amesema Mbughuni.
Ameongeza, ndiyo maana dira yao inasema “tanzania yenye mafundi stadi mahiri na wakutosha” na kwamba kauli mbiu yao inasema “ufundi stadi, fursa kama zote kwa watu wote.
MSISITIZO WA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA UTOAJI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI.
Amesema, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, elimu ya ujuzi imepewa kipaumbele kama muhimili wa ajira na maendeleo, na kwamba katika hotuba yake Rais Samia aliyoitoa Bunge tarehe 14 Novemba 2025, alisisitiza kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia vyuo vya ufundi stadi na kuunganisha mafunzo na miradi mikakati kama SGR, bandari, uchumi wa bluu, madini na gesi.
“Kauli hii inathibitisha kuwa kijana anayepata ujuzi leo anapata ajira kesho, VETA ndiyo chombo kikuu cha kutekeleza maono hayo, na sisi VETA Shinyanga katika kuunga mkono kauli ya Mheshimiwa Dkt Samia Saluhu Hassan, katika kuwajengea vijana kesho iliyobora zaidi, tunakauli mbiu yetu isemayo “VETA Shinyanga ,Kazi mkononi” ikimaanisha kuwa muhitimu wa Chuo cha VETA Shinyanga ahitimu akiwa hana mwelekeo, bali anatoka akiwa na ujuzi unaomuwezesha kuajiriwa au kujiajiri na kuanzisha shughuli zake za kiuchumi kulingana na ujuzi alioupata,” amesema Bughuni.
Juhudi za VETA Shinyanga katika kupanua fursa kwa vijana.
Amesema, katika kuunga juhudi za Serikali ya awamu ya sita, VETA Shinyanga imedhamiria kuendelea kwa kuhakikisha inatoa fursa za Mafunzo kwa vijana.
Kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi.
Amesema, kwa sasa Chuo kinaendelea kuhamasisha vijana wengi zaidi katika wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga, ili wajitokeze kujiunga na Mafunzo ya muda mrefu na muda Mfupi katika fani mbalimbali zilizopo Chuoni hapo.
Mbughuni amesema, kabla ya upanuzi wa miundombinu ya chuo, uwezo wa chuo ulikuwa ni kudahili wanachuo wapatao 400 wa kozi za muda mrefu, na wanafunzi chini ya 1,200 kwa mwaka.
Amesema, baada ya upanuzi wa miundombinu ya chuo uliofanyika mwaka 2010 kupitia mradi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Udahili umeongezeka na kufikia wanafuzi 545 wa kozi za muda mrefu, na wanafunzi zaidi ya 3,000 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.
“Ubora wa mafunzo yanayotolewa na VETA Shinyanga, umepelekea kupata wanafunzi wa kozi za muda mfupi kutoka nchi zote za Afrika mashariki na kati, hivyo kupelekea wahitimu wa kozi hizi kupata ajira ndani na nje ya nchi na kuchangia katika uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati,” amesema Mbughuni.
Amezitaja nchi hizo za Afrika Mashariki na Kati kuwa ni Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudani ya Kati, Kongo, Iraq, Elitrea na visiwa vya Comoro.
Kuanzisha kozi mpya kulingana na soko la ajira.
Amesema, VETA Shinyanga imedhamiria kueendelea kutoa kozi zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira kama Umeme wa Majumbani na Viwandani, Uashi, Useremala, Ushonaji na Ubunifu wa Mavazi, Uchomeleaji na Uundaji Vyuma.
Kozi zingine ni Ufundi wa mitambo mizito, Uhazili na Tehama, Ukataji, ung’arishaji na uchongaji wa madini vito, Ufundi Bomba na kwamba kozi hizo zimeboreshwa ili ziendane na shughuli za kiuchumi za eneo la Shinyanga kama madini, ujenzi na biashara ndogo ndogo, kulingana na mahitaji ya soko la ajira.
Amesema, pia wameanzisha kozi mpya za ufundi magari, Umeme wa Magari na Utengenezaji na Ukarabati wa miundombinu ya Barabara.
Kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa makundi maalumu.
Mbughuni amesema, Chuo hicho katika kutoa Mafunzo ya ufundi Stadi, kinapokea na kutoa mafunzo kwa makundi maalumu kwa vijana wasio na ajira, Wanawake na vikundi vya ujasiriamali.
Aidha, amesema kupitia Program ya Wanawake na Samia ilikuwa na washiriki 368, pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) ulikuwa na washiriki 20(me 16 na ke 04).na kwamba Wote hao wamesoma fani mbalimbali ili kuwa patia ujuzi na kiuchumi nahata kuweza kujiajiri au kuajiriwa, na hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ushirikiano wa viwanda na taasisi katika utoaji mafunzo.
Amesema, katika kuwawezesha vijana kupata Mafunzo yenye ubora na yenye kuzingatia soko la ajira, Chuo hicho kimeendelea kushirikiana vyema na viwanda na taasisi mbalimbali nchini katika kuwapatia wanafunzi Mafunzo kwa Vitendo (IPT) na mfumo wa Uanagenzi pacha (DATS) ambapo wanafunzi hupata Mafunzo ya mahali pa kazi.
Amezitaja taasisi hizo ni kama migodi, Karakana binafsi, Makampuni ya ujenzi, taasisi za umma, na hivyo kuwaongeza uwezekano wa kuajiriwa baada ya mafunzo.
Urasimishaji Ujuzi (Recognition of Prior Learning)
Mbughuni amesema, katika kuhakikisha wanaunga juhudi za Rais Samia, kwamba wanaendelea kutoa fursa kwa mafundi waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi, ambapo Chuo huwafanyia tathmini ya umahiri wao kulingana na fani zao, na kisha kuwapatia vyeti vinavyotambulika kitaifa.
“Fursa hii huwasaidia kupata ajira rasmi au kushiriki zabuni mbalimbali nchini, mfano zabuni za ujenzi wa shule, hospitali na shughuli nyingine mbalimbali zinazotolewa na serikali,” amesema Mbunghuni.
Uboreshaji wa Miundombinu na Vifaa.
Amesema, Serikali kupitia VETA Makao Makuu, imeendelea kuboresha karakana, madarasa na ununuzi wa zana za kufundishia na kujifunzia ili kuongeza ubora na idadi ya wanafunzi wanaopokelewa.Hii inawezesha vijana wengi zaidi kuweza kujiunga na Mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo chetu.
Uhamasishaji wa Elimu ya Ufundi Stadi.
Amesema, pia Chuo cha VETA Shinyanga kupitia mikutano ya kijamii, maonesho, na vyombo vya habari kimeendelea kuhamasisha jamii kutambua kuwa ufundi stadi ni fursa ya ajira na kujitegemea.
Kupokea waombaji wenye elimu ya juu.
Amesema, chuo hicho kimedhamiria kutoa fursa za mafunzo kwa vijana, na kwamba kinapokea waombaji wote wenye mahitaji maalumu bila ubaguzi na huwapa ushauri wa kitaaluma ili wachague fani zinazoendana na uwezo wao.
“Chuo chetu kinawapokea wahitimu wa elimu ya juu wanaotaka kuongeza ujuzi wa vitendo (hands-on skills) ili kujiongezea uwezo wa kuajirika au kujiajiri, ili kuwa saidia kupata stadi za kiufundi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira hususan wale waliokaa muda mrefu wakisubiri ajira za serikali,” amesema Mbughuni.
Uimarishaji wa ubora wa mafunzo.
Amesema chuo hicho kimeendelea kununua vifaa na mitambo mbalimbali, kufanya mashirikiano na Mafundi mahiri na viwanda katika utoaji wa mafunzo.
CSR.
Amesema, chuo hicho katika kurudisha kwa jamii, wamekuwa wakitengeneza miundombinu ya barabara ambazo zimekuwa hazipitiki mtaani, ikiwa pia ni sehemu ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Wito kwa vijana.
Ametoa wito kwa vijana, kwamba wajiunge na chuo hicho ili wapate ujuzi, ambao utawasaidia hata kujiajiri wenyewe kuliko kukaa vijiweni wakilalamika hakuna kazi.
“VETA Shinyanga imeendelea kuamini ya kuwa dunia ya leo haihitaji vyeti pekee, bali inahitaji uwezo wa kufanya kazi kwa kuwa ujuzi ni mtaji, ajira na hujenga ujasiri wa kujitegemea na kujenga heshima,” amesema Mbughuni.
Nao baadhi ya vijana ambao wanasoma chuo hicho akiwamo Upendo Zacharia ambaye amemaliza masomo yake ya Shahada “Degree’ Socialogy katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) mwaka 2025, amesema ameamua kusomea fani ya mitambo ili kujiongezea ujuzi kuwendana na ushindani wa soko la ajira.
Upendo Zacharia.
Naye Mwanafunzi Ezrom Shadrack ambaye amemaliza Shahada ya Elimu, Utawala na Uongozi katika chuo cha Dodoma (UDOM) mwaka 2023, amesema amechukua fani ya mitambo katika Chuo cha VETA, na kutoa wito kwa vijana wasibwete kulia hawana ajira, bali wajiunge na VETA ili wapate ujuzi na kuingia kwenye soko la ushindani wa ajira na hata kujiajiri wenyewe.