Na Marco Maduhu, SHINYANGA
JUMUIYA ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Wilaya ya Shinyanga imewataka wazazi kutosahau wajibu wao wa malezi ya watoto kwa kuwachia wadada wa kazi pekee, jambo ambalo wakati mwingine limekuwa likisababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili.
Hayo yameelezwa Machi 8, 2026 wakati jumuiya hiyo ilipotoa elimu kwa jamii kuhusu kupinga vitendo vya ukatili katika Kanisa la EAGT Majengo Mapya Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Shinyanga Maryester Nyarusanda, amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakijikita zaidi katika shughuli za kutafuta kipato na kusahau kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao.
Amesema hali hiyo imewapa nafasi baadhi ya wadada wa kazi kufanya vitendo visivyofaa kwa watoto bila wazazi kugundua mapema.
“Tumewahi kusikia kisa cha familia moja ambapo mdada wa kazi alikuwa na tabia ya kuwapa watoto chakula kilichochanganywa na hedhi kwa muda mrefu bila wazazi kujua. Tukio hilo lilikuja kugundulika baada ya watoto kuanza kudhoofika kiafya,” amesema Nyarusanda.
Amesema, matukio kama hayo yanaonyesha umuhimu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto wao, badala ya kuwaachia wadada wa kazi pekee bila ufuatiliaji wa karibu.
Kwa upande wake Katibu wa SMAUJATA wilayani humo Hasna Maige, amewataka pia wazazi kuepuka tabia ya kuwalaza watoto pamoja na wageni hasa wa kiume, akieleza kuwa hali hiyo wakati mwingine huwapa nafasi baadhi ya watu kuwafanyia watoto michezo michafu.
Aidha, amewahimiza wanandoa kuishi kwa kuheshimiana na kudumisha maelewano katika familia, ili kuimarisha amani ya ndoa na kuepuka migogoro inayoweza kusababisha vitendo vya ukatili majumbani.
Maige pia ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vya ukatili katika jamii, ikiwamo kwa viongozi wa serikali za mitaa, ili hatua zichukuliwe mapema kabla ya kuleta madhara.
Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT Majengo Mapya Manispaa ya Shinyanga David Lugema, amewataka wazazi kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili, sababu sasa hivi dunia imeharibika, kutokana na shetani kutafuta kuabudiwa kwa nguvu.
Amewasihi pia wazazi wawe makini, na simu za mkononi kwa kutowaachia watoto wao kuzichezea, ili kuepuka kuathiriwa na maudhui yasiyofaa kwa umri wao na kuwa haribu kimaadili.
Katika hatua nyingine amesema kwenye mfungo wa siku 40 wa Kanisa hilo, wameliombea Amani taifa, pamoja na viongozi kuwa na afya njema wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
TAZAMA PICHA👇👇
Mchungaji wa Kanisa la EAGT Majengo Mapya Manispaa ya Shinyanga David Lugema akizungumza.
Mchungaji wa Kanisa la EAGT Majengo Mapya Manispaa ya Shinyanga David Lugema akizungumza.
Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Shinyanga Maryester Nyarusanda akitoa elimu ya ukatili.
Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Shinyanga Maryester Nyarusanda akitoa elimu ya ukatili.
Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Shinyanga Maryester Nyarusanda akitoa elimu ya ukatili.
Katibu wa SMAUJATA wilayani humo Hasna Maige akitoa elimu ya ukatili.
Katibu wa SMAUJATA wilayani humo Hasna Maige akitoa elimu ya ukatili.
Katibu wa SMAUJATA wilayani humo Hasna Maige akitoa elimu ya ukatili.