` WAZIRI KATAMBI: HATUTAKUBALI SIASA ZA MIPASUKO, AMANI NA HAKI NI MSINGI WA MAENDELEO

WAZIRI KATAMBI: HATUTAKUBALI SIASA ZA MIPASUKO, AMANI NA HAKI NI MSINGI WA MAENDELEO

Na Suzy Butondo, Shinyanga

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga, Patrobas Katambi, amewashukuru wananchi wa Jimbo la Shinyanga pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kwa usimamizi mzuri wa uchaguzi uliowezesha kupatikana kwa madiwani, wabunge na Rais.

Katambi ameyasema hayo leo Februari 22,2026 wakati akizungumza na viongozi wa CCM kutoka kata zote za Wilaya ya Shinyanga katika mkutano maalum wa kuwashukuru wananchi kwa ushiriki wao mkubwa katika uchaguzi, ambapo amesema wananchi na viongozi wa CCM walifanya kazi kubwa ya kupiga kura na kuleta ushindi wa kishindo.

“Lengo la kuwaita leo ni kuwashukuru kwa kazi kubwa mliyoifanya, Niwaahidi tutasimamia miradi yote ya maendeleo na haki za wananchi wote bila kumuonea mtu yeyote, kwani tunasimamia misingi ya kikatiba,” amesema Katambi.

Ameeleza kuwa yeye pamoja na madiwani na wabunge wana jukumu la kuwaletea wananchi maendeleo na kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi. Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi za maendeleo, hivyo amewataka wakandarasi kufanya kazi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

“Sitakubaliana na mkandarasi yeyote atakayochelewesha kazi bila sababu maalum. Fedha zipo, kazi ifanyike,” amesisitiza.

Katambi pia ameeleza kuwa hatakubali siasa za mipasuko, chuki za kisiasa au kidini, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo na lazima ilindwe kwa maslahi ya wananchi wote.

“Tunataka haki na amani kwa kila mmoja. Changamoto zozote za kisiasa au kidini tutazishughulikia kwa mujibu wa sheria,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewataka wananchi na viongozi wa CCM kumuombea Waziri Katambi, akieleza kuwa anatekeleza jukumu kubwa la kitaifa linalohitaji maombi na mshikamano.

Amesema ushindi mkubwa uliopatikana Shinyanga Mjini umeleta matunda makubwa kwa Mkoa wa Shinyanga, na amewataka wananchi kuendelea kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Tuache ushabiki wa majungu,Uchaguzi umeisha, sasa ni wakati wa kuwa wapambe wa maendeleo  CCM ni moja, na lazima tuendelee kulinda amani ya nchi yetu,” amesema Mlolwa.

Aidha, amewataka madiwani wote wa Mkoa wa Shinyanga kwenda kwa wananchi kuwashukuru kwa kuwaamini na kuwachagua kwa kura nyingi, akisisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi kurejesha shukrani kwa wananchi waliowapa dhamana.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464