Na mwandishi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amewataka wananchi kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa uhai, maendeleo na ustawi wa Taifa.
Akizungumza Februari 22, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, Katambi amesema kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa amani na utulivu.
Alionya watu wenye nia ovu dhidi ya Serikali na Taifa kuacha mara moja vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi, akisisitiza kuwa matukio yaliyotokea Oktoba 2025 yasirudiwe tena.
“Amani ya nchi ndiyo msingi wa hatua zote za maendeleo na ustawi wa kila mmoja wetu. Ni wajibu wa kila mwananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda tunu hii, kwa kuwa sote ni wanufaika wa amani,” amesema Katambi.
Aidha, amewataka wananchi kuacha tabia ya kusambaza na kufurahia maudhui yanayochochea uvunjifu wa amani kupitia mitandao ya kijamii au majukwaa mbalimbali, hasa yanayohusisha imani za dini, vyama vya siasa na ukabila, kwa maslahi binafsi au kwa kushawishiwa kwa rushwa.
Kwa upande mwingine, Waziri huyo amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma kufanya kazi kwa uzembe, akisema hali hiyo inakwamisha utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema hatasita kutumia mamlaka yake kusimamia nidhamu kwa watumishi watakaobainika kuchelewesha au kukwamisha huduma kwa wananchi.
“Nitatumia mamlaka niliyonayo kuhakikisha watumishi wa umma wanaotekeleza majukumu yao kwa uzembe na kuichonganisha Serikali na wananchi wanachukuliwa hatua stahiki,” amesisitiza.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Serikali za mitaa, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wa Manispaa ya Shinyanga.