.jpg)
Uwekezaji wa kihistoria wa Shilingi bilioni 700 katika upanuzi wa kiwanda cha Kilombero Sugar siyo tu habari ya takwimu za serikali, bali ni mlango mpya wa fursa kwa vijana wa Kitanzania. Huu ni ubia wa kimkakati kati ya Serikali na mwekezaji unaolenga kuifanya Tanzania ijitosheleze kwa sukari, lakini nyuma yake kuna "mchongo" mkubwa kwa vijana wenye maono.
Akizungumza hivi Februari 24, 2026 mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, amebainisha kuwa uwekezaji huu unakwenda kuwa mwarobaini wa kilio cha muda mrefu cha wakulima wa miwa.
Kwa miaka mingi, wakulima wa miwa Kilombero walikabiliwa na changamoto ya miwa yao "kukaa shambani" na kupoteza ubora kutokana na uwezo mdogo wa kiwanda wa kuchakata mazao hayo.
Hivyo uwekezaji huu unamaanisha kiwanda sasa kina "tumbo" kubwa la kutosha kupokea kila bua la muwa linalozalishwa. Hii inahakikisha fedha za mkulima hazipotei na inabadilisha kilimo kutoka cha "kujikimu" kwenda cha "biashara yenye faida".
Wakati Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, ameweka wazi kuwa uwekezaji huu unakwenda kufuta changamoto za muda mrefu za wakulima, Mwenyekiti wa Bodi ya Sukari, Prof. Kennedy Bengesi, amesisitiza kuwa uwekezaji huoni muhimu kwa sababu unaleta utulivu wa bei ya sukari mtaani na kukuza uchumi wa ndani, jambo linaloongeza mzunguko wa fedha katika eneo husika.
Faida nyingine ya uwekezaji huo unaokuja na mitambo ya kisasa ya uzalishaji ni kwa kijana aliyesomea ufundi (VETA au Vyuo Vikuu), kuingia kwenye mfumo wa uchumi wa viwanda. Kiwanda kitahitaji wahandisi, wataalamu wa mitambo (automation), na wataalamu wa maabara. Hii siyo tu ajira, bali ni nafasi ya kupata utaalamu wa kimataifa (Technical Expertise).
Aidha kama kijana, hana haja ya kuajiriwa kiwandani moja kwa moja anaweza kuingia mkataba kama mkulima mdogo (Outgrower) ukiwa na uhakika wa soko la miwa yake huku akitumia utaalamu wa washauri wa kilimo wa kampuni kuongeza tija ili miwa yake ikubalike kiwandani.
Pia uwekezaji huo unafanya maajabu katika mnyororo mzima wa soko na usafirishaji Kiwanda kikizalisha sukari nyingi, inahitaji kusambazwa nchi nzima na hivyo kutengeneza fursa ya kutoa huduma za malori ya kusafirisha miwa kutoka shambani au kusambaza bidhaa ya mwisho sokoni.
Uwakala na Usambazaji: Vijana wanaweza kuchangamkia fursa za kuwa miongoni mwa wasambazaji wa sukari na bidhaa nyingine zitokanazo na miwa.
Faida nyingine ni ujasiriamali na huduma saidizi kama chakula na malazi yaani kuwapo kwa fursa ya kutoa huduma za kutoa chakula (Catering) kwa wafanyakazi wa kiwandani na ujenzi wa nyumba bora za kupanga;huduma za ufundi kama gereji za matengenezo ya magari hadi huduma za tehama.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464