
OFISI ya Msajili wa Hazina imetoa takwimu zinazoashiria mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini Tanzania, ikibainisha kuwa kampuni ambazo serikali ina hisa chache zimeimarika na kuwa chachu ya ukuaji wa pato la taifa.
Mafanikio hayo yanatajwa kuwa ni matokeo ya moja kwa moja ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), jambo ambalo limeongeza ufanisi na uwajibikaji katika uendeshaji wa kampuni hizo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kuelekea Jukwaa la Wakurugenzi litakalofanyika Arusha, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, alisema kuwa gawio kwa serikali limepaa kutoka Sh bilioni 58.26 mwaka 2020 hadi kufikia Sh bilioni 266.52 mwaka 2024.
Ongezeko hilo la asilimia 357 ni kielelezo tosha kuwa kampuni ambazo serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 51 sasa zinaendeshwa kwa faida kubwa na kuchangia mapato ya ndani yanayosaidia kugharamia miradi ya maendeleo.
Ukuaji huu wa mapato hauishii kwenye gawio pekee, kwani takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka minne, kampuni hizo zimechangia takribani Sh trilioni 3.67 kama kodi ya mapato ya kampuni. Aidha, thamani ya uwekezaji wa serikali katika taasisi hizi imepanda kutoka Sh bilioni 821.51 hadi kufikia Sh trilioni 1.94, sawa na ongezeko la asilimia 136.
Ongezeko hili la thamani linaashiria kuwa rasilimali za watanzania ziko salama na zinaendelea kuzalisha tija tofauti na miaka ya nyuma ambapo mashirika mengi yalikuwa yakijiendesha kwa hasara.
Kwa upande wa hatima ya ajira kwa vijana, kuimarika kwa sekta hizi za kibiashara kunatoa mwanga wa matumaini kwa maelfu ya wahitimu wanaoingia sokoni kila mwaka.
Kupitia upanuzi wa sekta za benki, madini, nishati, na mawasiliano, nafasi mpya za kazi zinatengenezwa, huku ushirikiano wa sekta binafsi ukisaidia vijana wa Kitanzania kupata ujuzi wa kisasa na teknolojia ya ushindani. Hii inapunguza mzigo wa serikali kuwa mwajiri mkuu na badala yake kutengeneza mazingira ambapo sekta binafsi inakuwa injini ya ajira.
Hatima ya uchumi wa Tanzania sasa inaonekana kuwa imara zaidi, kwani mfumo huu wa usimamizi unajenga uchumi shindani na jumuishi.
Kwa kuimarisha uwezo wa bodi za wakurugenzi na watendaji wakuu kupitia majukwaa ya kimkakati, serikali inahakikisha kuwa kampuni hizi zinaenda sambamba na mabadiliko ya soko la dunia. Hali hii inajenga imani kwa wawekezaji wa nje na ndani, huku ikihakikisha kuwa huduma za kijamii kama afya na elimu zinaendelea kuimarika kutokana na kodi na gawio zinazopatikana kutoka kwenye uwekezaji huo wenye tija.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464