` ULEGA APELEKA USHAWISHI KWA WAHANDISI VIJANA KUTATUA KERO ZA TAIFA

ULEGA APELEKA USHAWISHI KWA WAHANDISI VIJANA KUTATUA KERO ZA TAIFA


WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka wahandisi nchini kuacha mazoea ya kuandika maandishi mengi yasiyo na tija na badala yake wajikite katika kubuni teknolojia zitakazotatua changamoto sugu za miundombinu na maendeleo nchini.

Akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) , Februari 23, 2026, Ulega alitangaza mkakati wa Wizara yake wa kuzawadia mawazo ya kibunifu yatakayotoa majibu kwa kero zinazoikabili jamii.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET), Waziri Ulega alitangaza zawadi ya shilingi milioni 10 kwa washindi watatu wenye mawazo bora. Alisema kuwa lengo si fedha pekee, bali ni kuwajengea uwezo vijana hao kwa kuwasajili kitaaluma, kuwafungulia kampuni, na kuwapa mikataba ya kiserikali ili kutekeleza mawazo yao.

“Dunia nzima ninyi wahandisi ndiyo mmekuwa chachu ya mabadiliko. Nchi yetu ina changamoto nyingi ambazo kwenu zinatakiwa kuwa fursa. Tunataka wahandisi watakaotatua kero na si wenye maandishi mengi yasiyo na mchango kwenye utatuzi,” alisema Ulega.

Alibainisha kuwa mshindi atakayewezeshwa kufungua kampuni atatengeneza ajira kwa wenzake na kuingizia taifa fedha za kigeni pale ubunifu wake utakapouzwa nje ya nchi. Aidha, aliongeza kuwa mpango huo unaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameshatenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji wa makundi ya vijana na wanawake nchini.

Ushindani huu unatarajiwa kuamsha ari kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuanza kufikiria miradi ya vitendo (practical solutions) itakayoweza kumaliza kero za ucheleweshaji wa miradi ya ujenzi, ubovu wa barabara, na ukosefu wa teknolojia rahisi za uzalishaji. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464