Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya uongozi ya kitaifa, Mkwasa alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwatoa vijana kwenye mawazo finyu ya kutegemea kuajiriwa na badala yake kuwajengea uwezo wa kuona na kuchangamkia fursa zinazowazunguka.
Alisisitiza kuwa uskauti wa sasa unalenga kuimarisha bongo za vijana na kuwapa mbinu za kisasa za kukabiliana na changamoto za maisha. Alisema kuwa kijana wa skauti anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa na nidhamu, uadilifu, na uthubutu wa kuanzisha miradi inayozalisha kipato.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu Msaidizi wa Programu za Vijana, Florence Asenga, alibainisha kuwa mitaala ya mafunzo hayo imeboreshwa ili kuwajengea vijana uwezo wa kuandaa na kuandika maandiko ya miradi (project proposals). Alisema ujuzi huo ni nyenzo muhimu itakayowawezesha vijana kupata mitaji na kuanzisha biashara au miradi ya ujasiriamali.
"Tunataka kijana wa skauti akitoka hapa awe na uwezo wa kujitegemea. Hatumpi tu ukakamavu wa mwili, tunampa ukakamavu wa akili utakaomsaidia kubuni miradi na kusimamia uchumi wake na wa jamii yake kwa ujumla," alisema Asenga.
Nao baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo kutoka mikoa mbalimbali, walieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa mwangaza mpya katika maisha yao.
Walisema kuwa yamefuta dhana ya zamani kuwa uskauti ni gwaride pekee, na sasa wamejipanga kurudi kwenye maeneo yao kuanzisha miradi ya pamoja itakayowasaidia kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
.jpg)