` MAPINDUZI YA KILIMO: TOSCI YAWAANDAA VIJANA KUMILIKI UCHUMI WA MBEGU

MAPINDUZI YA KILIMO: TOSCI YAWAANDAA VIJANA KUMILIKI UCHUMI WA MBEGU

KATIKA juhudi za kuhakikisha sekta ya kilimo inachangia kikamilifu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewataka vijana wanaochipukia katika biashara ya pembejeo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajikite katika weledi.

Rai hiyo iliyotolewa na Mkaguzi na Mtafiti wa Mbegu kutoka TOSCI, Dk. Neema Yohana, kwenye mafunzo maalumu kwa wajasiriamali vijana wanaotarajia kuwa mawakala wa mbegu na pembejeo inaonesha juhudi za serikali katika kuhakikisha inawandaa watu wake hasa vijana kushiriki katika uchumi wa nchi kwa kujitambua na kiuendelevu.

Alisema hayo kwa kuwa biashara ya mbegu ni mhimili wa usalama wa chakula, hivyo inahitaji watu stahiki ili kumlinda mkulima kuhakikisha anapata mavuno bora na wao wanakuwa katika mnyororo wa kunufaika.

Dk. Neema alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kuwawezesha vijana kujiajiri, lakini uwezeshaji huo unaendana na vigezo vya ubora. 

Alisema kuwa TOSCI, kwa kushirikiana na wadau wengine, imedhamiria kuwajengea uwezo vijana hao ili waweze kusambaza mbegu kwa kufuata misingi na taratibu za kisheria zilizowekwa.

Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Taasisi ya Kukuza na Kuendeleza Mifumo ya Kimasoko (AMDT) kupitia ufadhili wa Shirika la AGRA, yamelenga mradi wa Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture (YEFFA). 

Mradi huu unatajwa kama daraja la kuelekea uchumi wa kati wenye viwanda, ambapo kijana hatakuwa muuzaji wa bidhaa pekee, bali mshauri wa kitaalamu kwa mkulima.

Mtaalamu kutoka AMDT, Delta Shila, alieleza kuwa jumla ya vijana 40 kutoka mikoa ya Singida, Manyara, Dodoma, Iringa, na Morogoro wamepata mafunzo hayo kwa siku nne. Aliongeza kuwa lengo ni kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ambapo mbegu na viuatilifu vitawafikia wakulima vikiwa katika hali ya ubora unaokubalika kimataifa.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu hiyo ni mkombozi dhidi ya changamoto walizokuwa wakizipata huko nyuma. 

Naomi Munuo kutoka Singida na Sharifa Kabandika kutoka Bahi, walikiri kuwa wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara kwa kununua mbegu zisizoendana na tafiti za udongo, jambo ambalo mafunzo hayo yanakwenda kulitatua.

Hatua hii ya TOSCI na wadau wake inatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwashirikisha vijana katika sekta ya uzalishaji. 

Chini ya falsafa ya uwajibikaji, vijana sasa wanatakiwa kutumia fursa hizo kwa uadilifu mkubwa, wakitambua kuwa soko la kilimo linahitaji weledi na si ujanja-ujanja ambao umekuwa ukiwarudisha nyuma wakulima kwa muda mrefu. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464