
Na Neema Sawaka,Geita
Zaidi ya kilo 6,750,000 za pamba mbegu zinatarajiwa kuzalishwa katika wilaya za Mbogwe na Bukombe mkoani Geita kupitia Chama Kikuu cha Ushirika cha Mbogwe na Bukombe (MBCU).
Matarajio hayo yatafikiwa endapo wakulima watachukua na kupanda mbegu zote zilizotolewa, hatua itakayoongeza uzalishaji, na kipato cha wakulima kwa kukuza uchumi wa chama cha ushirika.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika wilayani Mbogwe, Mwenyekiti wa MBCU, Said Tangawizi, amesema uzalishaji huo unatarajiwa kupatikana kutoka kwenye ekari 4,500 zitakazolimwa na wakulima kutoka halmashauri za Mbogwe na Bukombe.
Amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa chama wa kuimarisha zao la pamba na kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja na juhudi zao za uzalishaji.
Tangawizi ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, chama hicho kinatarajia kuanza kuchambua pamba katika kiwanda cha MBCU LTD kilichopo Masubwe wilayani Mbogwe, kwa lengo la kuongeza mapato ya wakulima wa pamba na kuinua uchumi wa chama.
Kutokana na mpango huo, chama kinatarajia kununua jumla ya kilo 5,000,000 za pamba zenye thamani ya shilingi 9,552,979,000 kutoka kwa wakulima wa Mbogwe, Bukombe na maeneo mengine ya jirani.
Hata hivyo, amesema chama kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kuchelewa kupatikana kwa mikopo ya kununulia pamba kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
“Changamoto nyingine ni kuporomoka kwa soko la pamba nyuzi na pamba mbegu pamoja na kupanda kwa gharama za uendeshaji na uchambuaji wa zao hilo, hali inayosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli,” amesema Tangawizi.
Changamoto nyingine ni kuyumba kwa soko la pamba nyuzi na pamba mbegu sambamba na kupanda kwa ghalama za uendeshaji na uchambuzi wa pamba kunakosasbabishwa na kupanda kwa ghalama za petrol " amesema said Tangawizi.
Akielezea mafanikio ya msimu uliopita, Meneja wa MBCU, Paulo Samweli, amesema chama kimefanikiwa kutoa ajira kwa wanawake na vijana katika kipindi chote cha uzalishaji wa pamba, pamoja na kuhakikisha malipo ya wakulima yanafanyika kwa wakati, jambo lililosaidia kuongeza imani ya wakulima kwa chama hicho.
Kwa upande wake, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Geita, Doreen Mwanri, amewashauri wanaushirika kuachana na kilimo cha mazoea na kuhamia kwenye kilimo cha kisasa ili kuongeza tija na faida.
“Baadhi ya wakulima bado mnalima kwa kutumia jembe la mkono, hali inayowachosha na kuwakatisha tamaa. Ni wakati wa kuachana na mbinu hizo na kulima kilimo chenye tija ili tukipende kilimo na kinufaike,” amesema Mwanri.
Aidha, amewakumbusha wanaushirika kuzingatia Sheria za Ushirika, hususan katika suala la ununuzi wa hisa, ili kuendelea kukidhi sifa zilizoainishwa kisheria.
Mkutano huo mkuu wa MBCU pia umejadili namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo ununuzi wa hisa kwa baadhi ya wanachama, utunzaji wa mazao, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya chama, serikali na wadau wa sekta ya kilimo kwa lengo la kuendeleza zao la pamba kwa manufaa ya wakulima na taifa kwa ujumla

.jpeg)
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464