` UMOJA NA MARIDHIANO NDIO SIRI YA USTAWI VIJANA WAKUMBUSHWA

UMOJA NA MARIDHIANO NDIO SIRI YA USTAWI VIJANA WAKUMBUSHWA

LEO, Visiwa vya Unguja na Pemba vinasherehekea miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964. Huu ni wakati wa kutafakari maneno ya Rais wa Kwanza, Shehe Abeid Amani Karume, aliyewahi kusema: "Uhuru huondoa unyonge, huondoa dhuluma na shida... serikali haiwezi kuwa ya kinyang'anyiro, lazima iwe na macho."

Leo, macho ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais Dk. Hussein Mwinyi yanaonekana wazi kupitia matunda ya amani, umoja wa kitaifa, na maridhiano ambayo yamekuwa injini ya kasi ya maendeleo ambayo Zanzibar haijawahi kuishuhudia huko nyuma.

Maendeleo ya Elimu: Kiwanda cha Kesho ya Vijana Mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ni ushahidi tosha wa faida za utulivu nchini. Katika kipindi kifupi, Serikali imejenga shule 35 za ghorofa, na hivi karibuni Dk. Mwinyi amezindua Shule ya Msingi Muungano huku akitangaza mkakati wa kuongeza bajeti ya elimu kufikia Sh trilioni moja.

Kupitia mkataba wa Sh bilioni 240 na Benki ya CRDB, shule nyingine 29 za ghorofa zinajengwa katika maeneo ya Unguja na Pemba kama vile Fuoni, Jumbi, Micheweni na Kiuyu Minungwini. 

Haya ni maendeleo yanayogusa moja kwa moja maisha ya vijana, yakitengeneza mazingira bora ya kusoma na kuondoa kero ya msongamano madarasani. Aidha, ajira kwa walimu zaidi ya 1,700 kwa mwaka mmoja ni kielelezo cha namna amani inavyofungua milango ya uchumi.

Amani ndio Mtaji wa Utalii na Miundombinu

Zanzibar imeweka rekodi mpya katika utalii kwa kupokea watalii zaidi ya 106,000 kwa mwezi mmoja (Julai 2025). Maelfu ya vijana wanapata ajira katika sekta hii ya hoteli na huduma. Mafanikio haya yasingewezekana bila kuwepo kwa umoja wa kitaifa na maridhiano yanayohakikisha kuwa kila mgeni anajihisi salama.

Vilevile, ujenzi wa barabara za kisasa kama ya Kitogani-Paje ( Kilometa 13.2) na uimarishaji wa viwanja vya ndege ni matokeo ya nchi iliyotulia. Amani ndiyo iliyofanya Benki ya Dunia na wadau wengine kuwa na imani ya kuwekeza mabilioni ya fedha nchini kwetu.

Onyo kwa Vijana: 

Msidanganywe, Amani ndio Suluhu Licha ya mafanikio haya, vijana wanapaswa kuwa macho. Kuna watu wanaoweza kutumia mitandao na majukwaa ya kisiasa kuwapotosha na kuwahamasisha kuingia kwenye mivutano inayoweza kuvuruga utulivu huu. Ujumbe kwa vijana ni wazi: Amani haina mbadala.

Shida za ajira, mitaji na maendeleo hazitatuliwi kwa kelele, vurugu, au chuki, bali hutatuliwa kupitia utulivu unaoruhusu serikali kujenga shule, kuajiri walimu, na kuvutia wawekezaji.

 Ukikubali kudanganywa na kuvuruga amani, unaharibu miundombinu inayojengwa kwa kodi yako na unaziba milango ya fursa zako mwenyewe.

Zanzibar inapoadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi, Watanzania tujikumbushe kuwa hili ni taifa letu sote. Maridhiano na umoja wa kitaifa ndio "dau" linalotuosha unyonge na kutupeleka kileleni. Vijana simameni kidete kulinda amani ya nchi yenu, fanyeni kazi kwa juhudi, na muwe walinzi wa miundombinu ya elimu na afya inayojengwa na serikali yenu. 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464