` TUME YA UCHUNGUZI WA UVUNJIFU WA AMANI YAKUTANA NA WADAU WAMO SUMAYE,MADELEKA

TUME YA UCHUNGUZI WA UVUNJIFU WA AMANI YAKUTANA NA WADAU WAMO SUMAYE,MADELEKA

Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 inaendelea na vikao vyake jijini Dar es Salaam ambapo katika hatua muhimu ya kuimarisha misingi ya utulivu wa kitaifa imekutana na viongozi waandamizi pamoja na wadau wa nyanja mbalimbali. 

Katika mfululizo wa mikutano hiyo iliyofanyika kuanzia Januari 29 hadi Januari 30 mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Tanganyika uliopo katika ofisi za Benki Kuu ya Tanzania Tume hiyo imepokea maoni na ushauri kutoka kwa Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Tluway Sumaye pamoja na Wakili wa kujitegemea Peter Madeleka.

Mchakato huo wa ukusanyaji wa taarifa haukuishia hapo kwani Tume pia imeketi na viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali ili kupata mtazamo wa kiraia kuhusu mnyororo mzima wa matukio hayo yaliyotikisa amani ya nchi. 

Miongoni mwa mambo makuu yaliyotawala majadiliano hayo ni pamoja na uchambuzi wa kina wa namna uvunjifu huo wa amani ulivyoanza na tathmini ya athari zilizojitokeza kwa wananchi pamoja na uharibifu wa mali na miundombinu muhimu. 

Aidha washiriki wa mikutano hiyo wametoa ushauri wa kitaalamu na kijamii kuhusu mbinu bora za kutumia ili kuepuka kujirudia kwa matukio kama hayo katika chaguzi zijazo.

Tume imesisitiza kuwa itaendelea na utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali wakiwemo waathirika wa moja kwa moja wa matukio hayo kwa lengo la kubaini kiini cha chanzo cha vurugu hizo. 

Taarifa hizi zote zinazokusanywa zinalenga kuandaa ripoti kamili itakayowasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kuchukuliwa kwa hatua zaidi za kisheria na kiserikali ili kulinda amani na ustawi wa Taifa.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464