Kaimu Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Juma amesema Tume hiyo itaendelea kulinda faragha za watoa ushahidi wanaofika katika mikutano ya tume hiyo sehemu mbalimbali nchini.
Profesa Ibrahim Juma amesema hayo leo Januari 24, 2026 alipokuwa akifungua mkutano wa Tume hiyo na Wananchi wa Wilaya ya Ubungo uliofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaam.
Profesa Juma amesema Tume hiyo imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya waathirika wa matukio hayo wakilalamika kuwa, taarifa zao binafsi walizoziwasilisha kwa Tume zinaonekana zikisambazwa mtandaoni bila ridhaa yao.
“Baadhi ya waathirika wanapigiwa simu wanaombwa kufanya mahojiano ‘interview’ na baadhi ya media jambo ambalo linawaletea msongo wa mawazo, ulinzi wa taarifa za binafsi na usiri na wengine imesababisha changamoto kwa familia zao,
“Kufuatia hali hiyo, utaratibu utakaoendelea kutumiwa ni Tume kueleza kazi zake kwa waandishi wa Habari na maudhui kwa ujumla lakini wakati wa kusikiliza waathirika waandishi hawatoruhusiwa ‘mtatupisha’” ameeleza Profesa.
Tume imesikiliza waathirika wa matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 kwa Mkoa wa Dar es Salaam katika Wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala na Ubungo. Itaendelea kusikiliza kwa sehemu nyingine ikiwemo Dodoma, Shinyanga, Ruvuma na Iringa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464
