TATIZO LA UDUMAVU LAPUNGUA SHINYANGA – RC MHITA
Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, ameongoza kikao cha tathimini ya mkataba wa lishe na bima ya afya kwa wote, na kubainisha kuwa tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano limepungua mkoani humo, kutoka asilimia 32.1 hadi asilimia 27.5.
Amebainisha hayo leo Januari 16, 2026, wakati akifungua kikao hicho, kilichohusisha viongozi wa serikali, wadau wa afya, lishe, madiwani, wakurugenzi wa halmashauri, wananchi pamoja na makundi maalumu.
Mbali na udumavu, Mhita amesema pia tatizo la ukondefu kwa watoto limepungua kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 1.3, huku watoto wenye uzito pungufu wakipungua kutoka asilimia 13.3 hadi asilimia 8.6, hatua inayodhihirisha mafanikio ya juhudi zinazochukuliwa katika kuboresha lishe ya watoto.
Amesema kupungua kwa viashiria hivyo kunatokana na jitihada za serikali na wadau mbalimbali kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi, pamoja na kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni, ili kuwajengea watoto msingi mzuri wa afya.
“Licha ya kupungua kwa tatizo la udumavu kutoka asilimia 32.1 hadi 27.5, bado kiwango hiki ni kikubwa, hivyo, tunapaswa kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa afua za lishe katika maeneo yetu,” amesema Mhita.
Aidha, amesema katika kipindi cha utekelezaji wa mkataba wa lishe cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2025 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wastani wa utekelezaji umefikia asilimia 55.4, hali iliyoonesha alama ya njano kwa viashiria vyote.
Kutokana na hali hiyo, Mhita amezitaka halmashauri zote mkoani humo kuongeza jitihada katika utekelezaji wa afua za lishe, ili kuhakikisha viashiria vyote vinafikia alama ya kijani, huku akisisitiza matumizi sahihi ya fedha zilizotengwa, hasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Pia amesisitiza umuhimu wa kusimamia na kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni, ili wanafunzi wapate lishe bora wakati wa masomo yao, sambamba na kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kuanza shule wanaandikishwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Musa Makungu, amesema utekelezaji wa mkataba wa lishe mkoani humo unaendelea vizuri, huku akisisitiza kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya afua za lishe zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Nao baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho, wametilia mkazo umuhimu wa utoaji wa chakula shuleni, wakisema ni chachu muhimu katika kuboresha lishe ya watoto, huku wakiahidi kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa jamii na kuchangia chakula kwa wanafunzi.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao hicho.
Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Shinyanga Mussa Makungu akiwasilisha taarifa ya lishe.
Meneja wa NHIF Shinyanga Isaac Katenda akiwasilisha wasilisho la Bima ya Afya.
Meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Magharibi Awanje Matenda akiwasilisha wasilisho la TIRA.