` TAHADHARI: WANAOSHANGILIA ANGUKO LA VENEZUELA, GREENLAND IMEWAFUNZA NINI?

TAHADHARI: WANAOSHANGILIA ANGUKO LA VENEZUELA, GREENLAND IMEWAFUNZA NINI?

WAKATI baadhi ya wachokonozi na wachambuzi wa mambo kijuujuu nchini Tanzania wakionekana kushangilia mbinu za kijeshi zilizotumiwa na Marekani kumng’oa Rais Nicolás Maduro nchini Venezuela, wenye akili na wataalamu wa kijiopolitika duniani wameanza kuona giza nene linalokuja.

Ujumbe ni mmoja: Usishangilie nyumba ya jirani inapoungua kwa petroli, maana upepo ukibadilika, kiberiti hichohicho kinaweza kuelekezwa kwako. Safari hii, kiberiti hicho kimegeukia Greenland, eneo linalomilikiwa na Denmark—mshirika mkubwa na mwanachama wa zamani wa NATO.

Kutoka Caracas hadi Greenland: Somo la Ubabe

Baada ya Marekani kufanikiwa operesheni yake nchini Venezuela, sasa macho ya utawala wa Rais Donald Trump yamehamia Greenland. Sababu inayotolewa ni ileile: 'Usalama wa Taifa wa Marekani.' 

Marekani inadai kuwa inahitaji udhibiti kamili wa Greenland ili kuweka mifumo yake ya kisasa ya ulinzi wa makombora (Golden Dome) dhidi ya Urusi na China. 

Hili limeleta mshtuko mkubwa nchini Denmark. Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, ametoa onyo ambalo halijawahi kutokea: "Shambulio dhidi ya Greenland litakuwa mwisho wa muungano wa NATO."

Hapa ndipo wenye akili wanapopaswa kupata picha kamili. Ikiwa Marekani inaweza kutishia kumeza ardhi ya mshirika wake wa karibu (Denmark) kwa sababu tu za kimkakati, ni nani aliye salama?

Hatari ya Kuvunjika kwa NATO

Muungano wa NATO, ambao umekuwa mwavuli wa usalama wa nchi za Magharibi tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, sasa uko shakani. Sheria za kimataifa zinaonekana kutoheshimiwa tena pale maslahi ya 'mwenye nguvu' yanapogusa ardhi ya mwingine.

Wachambuzi wa masuala ya usalama wanahoji: Ikiwa mwanachama mmoja wa NATO anaweza kumshambulia mwanachama mwenzake ili kupokonya ardhi, je, ibara ya 5 ya muungano huo inayolinda usalama wa wanachama ina maana gani tena? Huu ni usaliti wa kidiplomasia unaoonyesha kuwa 'urafiki' wa kimataifa unaweza kufutwa kwa usiku mmoja.

Ulaya Sasa 'Inajihami' kwa Maneno na Vitendo

Nchi za Ulaya, zikiongozwa na Ufaransa na Uingereza, zimeanza kuona kuwa haziwezi tena kuitegemea Marekani kama mlinzi. Zimeanza kutafakari mbinu za kujibu mapigo ikiwa Marekani itaendeleza ubabe wake dhidi ya Denmark:

Kufunga Bandari: Kukataa kutoa huduma za mafuta na chakula kwa meli za kivita za Marekani.

Hospitali za Kijeshi: Kukataa kupokea wanajeshi wa Marekani waliojeruhiwa vitani kwa ajili ya matibabu.

Kufunga Kambi: Kutaka kufungwa kwa kambi za kijeshi za Marekani zilizopo barani Ulaya.

Somo kwa Tanzania na Wachochezi Wetu

Kwa wale nchini Tanzania wanaodhani kuwa matukio ya Venezuela ni 'shoo' ya mbali, wanapaswa kuelewa kuwa mfumo wa sasa wa dunia hauna rafiki wa kudumu. 

Leo ni Venezuela, kesho ni Greenland, keshokutwa inaweza kuwa nchi yoyote ile yenye rasilimali au eneo la kimkakati linalohitajika na mataifa makubwa.

 Kitendo cha kushangilia na kusema eti aje kuleta demokrasia Tanzania ni ujinga wa kiwango cha lami, kwani akiamua kuja ni kwa ajili ya madini yetu kama anayataka kimkakati.

Kama Wenye akili huko wanakokaa wao wameshaona iweje waendelee kufyokoafyokoa: Dunia haina tena utulivu. Uhuru wa nchi ndogo na zenye nguvu za wastani unategemea umoja na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa. 

Kushangilia anguko la nchi nyingine kwa mbinu za nguvu ni kualika mfumo ambapo "mwenye nguvu ndiye mwenye haki" (Might is Right).

Tuendelee kulinda amani yetu na mshikamano wa kitaifa, huku tukijua kuwa nje ya mipaka yetu, dhoruba inayokuja haina ustaarabu.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464