
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na wimbi kubwa la mijadala kwenye mitandao ya kijamii inayoashiria kuwepo kwa mafarakano, shutuma, na kile kinachoitwa na wengi kuanza "kutubu" kwa makundi fulani ya wachochezi baada ya mambo kuwaendea mrama.
Mijadala hii, ambayo mara nyingi huambatana na lugha ya kejeli na dhihaka, inatoa picha halisi ya hali ya kijamii tunayopitia, ambapo umoja na staha vinaonekana kuanza kupotea na nafasi yake kuchukuliwa na roho za mafarakano na lugha za kutapatapa kwa wale waliokosa mwelekeo sasa wa uzalendo na utaifa.
Moja ya jambo linalojitokeza kwa nguvu ni malumbano yanayohusu malezi na heshima kwa mamlaka au wazazi. Jamii inahoji kizazi cha sasa ambacho kimekuwa na uthubutu wa kupindukia, kiasi cha kufikia hatua ya kukejeli misingi ya haki na wajibu.
Kuna hisia za wazi kuwa baadhi ya watu wanatumia kivuli cha kutafuta "haki" kufunika uovu, jambo linalopelekea msuguano mkubwa kati ya vizazi na hata ndani ya mifumo ya uongozi.
Inasikitisha kuona kuwa badala ya kujenga fikra mbadala, baadhi ya watu wamejikita katika usaliti na unafiki dhidi ya Tanzania, hali inayowafanya "wasambaratike" pindi maslahi yao binafsi yanapoguswa.
Aidha, kumeibuka tabia ya kutumia mambo mazito kama "imani" kujaribu kuwagawa watanzania. Watu hawa wanaotapatapa kama wafa maji wanatoa ishara wazi ya hatari inayotukumbusha kuwa tunahitaji ukombozi wa fikra na akili kuliko kitu kingine chochote.
Ni lazima sasa jamii ihoji mazingira na malezi ya watu wanaotoa hoja zisizo na msingi au zinazochochea chuki. Na hata sheria inapowakamata wanatakiwa kujua kwamba wamekamatwa kwa sababu ya kuvunja sheria zizazojenga kujali jamii.
Ni lazima tuseme ukweli mchungu: jamii yetu kwa sasa inatafunwa na kirusi hatari cha kejeli, dhihaka na ukosefu wa adabu uliokithiri, hususan katika nyanja za mitandao ya kijamii.
Yale ambayo zamani yalichukuliwa kama miiko na misingi ya utu, leo yamegeuka kuwa vichekesho. Tunashuhudia kizazi ambacho kimepoteza dira, na huu si ujanja, bali ni umaskini wa akili na ugonjwa wa kisaikolojia unaopaswa kukemewa kwa nguvu zote.
Chanzo cha janga hili ni mfumo wa malezi uliolala na uliojaa upendeleo usio na tija. Wazazi wa sasa wamekuwa waoga wa kuwakemea watoto wao, wakiamini kuwa "uhuru" unamaanisha kuacha mtoto akue kama mmea wa porini.
Matokeo yake ni watoto wanaoweza kumtukana mzazina hata kujihusisha na makundi maovu na kuharibu mali za umma. Ni lazima turejee kwenye misingi ya zamani: fimbo na nidhamu ni sehemu ya upendo.
Malezi ya "kuzaliwa kwa mimba za kupandikizwa" au kufuata mkumbo wa tamaduni za kigeni bila kuchuja, ndiyo yanayozalisha watu wasio na pointi bali kelele na matusi mitandaoni.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464