A.jpg)
.jpg)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mapinduzi makubwa katika safu ya ushauri wa ngazi ya juu kwa kuwateua viongozi waandamizi wastaafu wenye weledi uliotukuka ili kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Katika uteuzi huo uliotangazwa Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 10 Januari, 2026, Mheshimiwa Rais amemteua Makamu wa Rais mstaafu, Dkt. Philip Mpango, kuwa mshauri wake wa masuala ya uchumi na miradi, huku Waziri Mkuu mstaafu, Mhe. Kassim Majaliwa, akiteuliwa kuwa mshauri wa masuala ya jamii.
Ili kukamilisha safu hiyo, Rais amemuweka Profesa Palamagamba Kabudi kuwa kiungo mkuu atakayefanya kazi kwa karibu na washauri hao, hatua inayotajwa kulenga kuimarisha ufanisi wa serikali katika kuhudumia wananchi.
Uteuzi wa Dkt. Philip Mpango unakuja na hazina kubwa ya kitaaluma kwani yeye ni mbobezi mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika nafasi zake mbalimbali, Dkt. Mpango amewahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha na Mipango na Makamu wa Rais, ambapo alijipatia sifa ya kuwa msimamizi makini wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na mratibu wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Katika nafasi yake mpya ya ushauri, atatumia elimu yake ya uchumi na uzoefu wake wa kushirikiana na taasisi za kifedha duniani kuhakikisha miradi ya maendeleo inazalisha ajira na kukuza pato la taifa kwa kuzingatia hali ya uchumi wa sasa.
Kwa upande mwingine, Mhe. Kassim Majaliwa, ambaye ni mtaalamu wa elimu na uongozi akiwa na Shahada ya Elimu, anabeba jukumu la kushauri masuala ya jamii. Majaliwa ana uzoefu mkubwa kuanzia ngazi ya ualimu, ukuu wa wilaya hadi kuhudumu kama Waziri Mkuu kwa kipindi kirefu.
Utaalamu wake katika masuala ya elimu na uzoefu wake wa kufuatilia kero za wananchi vijijini utamsaidia Rais Samia kuhakikisha kuwa sekta za kijamii kama afya, maji na elimu zinaimarika.
Majaliwa atakuwa daraja muhimu katika kuhakikisha kuwa mipango ya serikali inatafsiriwa kuwa huduma bora kwa kila Mtanzania, huku akitumia uzoefu wake wa utawala kuleta suluhu za kijamii.
Katikati ya vichwa hivi viwili, Rais amemteua Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye ni mbobezi wa sheria mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani hiyo na uzoefu mpana wa kufundisha na kufanya utafiti.
Prof. Kabudi: Kiungo na Mstahimilivu wa Siasa za Dunia
Rais Samia amebainisha kuwa Profesa Palamagamba Kabudi atakuwa mratibu wa karibu wa washauri hao. Rais amemwelezea Profesa Kabudi kama "akili iliyotulia" inayoweza kushughulika na "vichwa vikubwa" (Dkt. Mpango na Majaliwa) huku akilinda maslahi ya nchi kwenye medani za kimataifa.
“Vile vichwa viwili vikubwa vinahitaji mtu aliyetulia anayeweza kudeal nao. Profesa (Kabudi) anaweza kwenda nao vizuri sana,” alisema Rais Samia.
Maana ya Uteuzi Huu kwa Taifa
Uteuzi huu si tu utekelezaji wa ahadi ya kampeni ya Mhe. Rais, bali ni kielelezo cha Ukuaji wa Taifa katika kujali utu na maendeleo. Kwa kuwakutanisha wataalamu hawa, Rais anajenga mfumo ambao:Unajali Utu: Maendeleo ya watu sasa yanashauriwa na kiongozi mwenye uzoefu wa nyanjani (Majaliwa).
Unajali Maendeleo: Miradi inashauriwa na bingwa wa mipango (Mpango) na Unajali Sheria na Diplomasia: Kila hatua inalindwa na mwanasheria mbobezi (Kabudi).
Hatua hii inadhihirisha ukomavu wa kisiasa wa Tanzania, ambapo uzoefu wa viongozi wastaafu unatumika kama hazina (Institutional Memory) ya kulifikisha taifa kwenye kilele cha uchumi wa kati na ustawi wa kweli kwa kila Mtanzania.