
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita, ametoa onyo kali dhidi ya kile alichokiita "kugota kifikiri" kwa baadhi ya taasisi na viongozi wa kisiasa wanaohamasisha mapinduzi ya kijeshi au kutegemea mataifa ya nje kuleta mabadiliko nchini Tanzania.
Akizungumza Januari 15, 2026, jijini Tanga katika ziara yake ya kikazi ya kukutana na viongozi na wajumbe wa jimbo la Tanga Mjini, Mchinjita amebainisha kuwa harakati za kisiasa zinapaswa kujikita katika kutengeneza mbadala wa kufikiri na uungwaji mkono wa umma badala ya kutamani njia za mkato zinazoweza kuliingiza Taifa katika majanga makubwa zaidi.
Akirejea matukio yaliyofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Mchinjita ameweka wazi kuwa hakushuhudia maandamano ya dhati yenye uongozi madhubuti wa kisiasa, bali aliona matukio yaliyokosa uratibu wa taasisi na vurugu.
Amewashangaa wadau wa kisiasa wanaofikiria kuwa mapinduzi ya kijeshi yanaweza kuwa nafuu kwa nchi, akisisitiza kuwa utawala wa kiraia, licha ya changamoto zake, unaruhusu uhuru wa kukosoa.
Amewakumbusha Watanzania kuwa chini ya uongozi wa kijeshi, matumizi ya nguvu na risasi ni sehemu ya utamaduni wa madaraka, na kwamba mataifa yaliyopitia njia hiyo yameshuhudia ukatili na unyama uliokithiri ambao hauruhusu hata nafasi ya kutoa maoni.
Mchinjita amekosoa vikali tabia ya baadhi ya wanaharakati wa mitandaoni na wanasiasa wanaoshabikia uingiliaji kati wa mataifa ya nje, kama vile Marekani, katika masuala ya ndani ya mataifa mengine.
Ameeleza kuwa ni kosa kubwa la kifikira kudhani kuwa maslahi ya Watanzania yatalindwa na viongozi wa kigeni, akitolea mfano wa miito ya kutaka mataifa hayo yaingilie kati Tanzania kama ilivyotokea Venezuela.
Amesema kuwa taasisi yoyote ya kisiasa inayotafuta "miujiza" kutoka nje imepoteza mwelekeo wa safari yake, kwani ukombozi wa kweli unapaswa kuanzia ndani kupitia kujipanga, kuhamasisha umma, na kujenga nishati ya wananchi wenyewe kuwa tayari kupigania mustakabali wao.
Kiongozi huyo ametoa mwito kwa viongozi wa kisiasa nchini kujitathmini na kuchukua hatua zitakazorejesha imani ya umma kwao.
Amesititiza kuwa jukumu la kiongozi ni kusimama mbele na kuongoza safari ya mabadiliko kwa vitendo na hoja mbadala zinazotekelezeka, badala ya kukaa na kusubiri matukio ya kusadikika.
Amesema kuwa harakati za kisiasa ni mchakato endelevu unaohitaji uvumilivu na mkakati wa muda mrefu, na kwamba ACT-Wazalendo itaendelea kusimamia njia za kidemokrasia na kistaarabu katika kudai haki na maendeleo ya Watanzania bila kuhatarisha amani ya nchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464