.jpg)
KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni mwamko mpya wa fursa za kidijitali, mtaalamu wa mifumo ya kompyuta na mitandao ya kijamii, Bazil Lokola, amewahimiza vijana nchini kubadili mtazamo wao juu ya matumizi ya mitandao na kuanza kuitumia kama chanzo rasmi cha ajira.
Akizungumza kwa hisia katika mjadala wa Meza Huru, Lokola amebainisha kuwa tasnia ya Teknolojia ya Habari (IT) na usimamizi wa majukwaa ya kijamii ina fursa lukuki zinazoweza kumtoa kijana kwenye lindi la umaskini, ikiwa tu atachagua kutumia utaalamu wake kwa tija.
Ushuhuda wa "Dili" la Instagram
Akitoa ushuhuda uliosisimua watazamaji wengi, Lokola alielezea namna ujuzi wake ulivyomlipa kiasi kikubwa cha fedha ndani ya muda mfupi, jambo ambalo hakulitegemea awali.
"Mimi kiutaalamu ni IT by Professional. Nakumbuka kuna mtu mkubwa kidogo alipoteza akaunti yake ya Instagram; mimi nilikuwa Dodoma na yeye yupo Dar es Salaam. Katika hangaika yake, akaniomba nimrudishie ile akaunti," alisimulia Lokola.
Aliongeza kuwa, baada ya kufanikisha kazi hiyo ya kitaalamu, malipo aliyoyapata yalikuwa ya kushangaza: "Nilipofanikisha lile jambo, alinilipa hela ambayo ni mara mbili ya ile niliyokuwa ninalipwa (mshahara wa kawaida)."
Amani na Matumizi Chanya ya Mitandao
Kwa kauli ya Mtaalamu huyo, vijana wanapaswa kuacha tabia ya kutumia mitandao ya kijamii kama majukwaa ya kuporomosha matusi, kudhalilisha watu au kuchochea ghasia, kwani vitendo hivyo vinawanyima fursa ya kuaminiwa na soko la ajira.
Ulimwengu wa sasa unahitaji vijana wabunifu wanaoweza kutatua changamoto za kidijitali.Kwa kurejesha akaunti iliyopotea au iliyovamiwa (hacked) ameonesha kwamba kuna hitaji kubwa kwa vijana kuwezesha watu maarufu, wafanyabiashara na taasisi, na hivyo ni nafasi ya kutengeneza fedha halali.
"Mitandao siyo sehemu ya malumbano tu; ni ofisi. Ukiwa na ujuzi na ukaamua kuutumia vizuri, utagundua kuwa kuna pesa nyingi ambazo hukuwahi kuzifikiria," alisema Lokola.
Wito kwa Wadau
Ushuhuda huu wa Lokola umekuja wakati kukiwa na mjadala mpana wa jinsi vijana wanavyoweza kujiajiri kupitia uchumi wa kidijitali (Gig Economy). Wadau wa maendeleo wanashauri kuwa elimu zaidi inahitajika ili kuwasaidia vijana kuelewa sheria za makosa ya mtandao na jinsi ya kulinda amani ya nchi wanapokuwa wakisaka fursa hizo.
Hilo linathibitishwa na Mkurugenzi wa Simu Kitaa Emmanuel Masoko."...leo hii ukiniambia mimi kuhusu mitandao ya kijamii siichukulii kama watu wengine wanavyoichukulia....mimi kwa upande wangu nikikutana na mtu yeyote ambaye yuko mwaka wa kwanza chuo anataka kuwa mfanyabiashara cha kwanza nitamwambia afungue ukurasa Instagram....." anasema Masoko.
Jukwaa hilo kwake ndilo limemfaidisha sana alikuwa anaangalia makosa ya wengine anasahihisha na kufanyha jukwaa lake kupanda chati haraka na kuwa ajira isiyokoma
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464