.jpg)
Serikali imezindua rasmi Jukwaa la Vijana (Youth Platform), chombo cha kisasa kinacholenga kuwa daraja imara kati ya vijana na Serikali katika kueleza changamoto, mahitaji, na matarajio yao kwa ajili ya mustakabali wa Taifa.
Uzinduzi huo ulifanyika jana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na viongozi waandamizi pamoja na wadau wa maendeleo ya vijana.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, alibainisha kuwa jukwaa hilo si tukio la siku moja bali ni nafasi ya kudumu ya mazungumzo ya kweli.
Alisisitiza kuwa Serikali inalenga kusikia sauti za vijana ili kuboresha sera, mipango, na programu za kuwawezesha kiuchumi na kijamii, hususan katika masuala ya ajira, biashara, teknolojia, na ubunifu.
Amani na Utulivu Katika Madai
Waziri Nanauka aliweka bayana kuwa nguvu ya vijana inapaswa kuelekezwa katika kujifunza utulivu na namna bora ya kuwasilisha mahitaji yao bila kuvuruga amani ya nchi. Alieleza kuwa Serikali iko tayari kusikiliza sauti za vijana, ilimradi ziwasilishwe kwa uwazi na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
“Nitoe rai kwa vijana kutumia jukwaa hili kwa uwajibikaji. Jifunzeni utulivu na amani katika kuwasilisha madai yenu. Serikali itasikiliza, itajifunza na kuboresha mifumo kwa kuzingatia sauti zenu, lakini ni lazima tufanye hivyo kwa kudumisha amani yetu,” alisema Nanauka.
Jukwaa Lifike Hadi Ngazi ya Kijiji
Katika kuhakikisha jukwaa hilo linakuwa na nguvu na ushawishi, Waziri Nanauka amewaagiza Maofisa Maendeleo ya Vijana nchini kuhakikisha kuwa mpango huo haubaki mijini pekee, bali unafika hadi ngazi za vijiji na mitaa.
Alisisitiza kuwa ili vijana wawe na sauti moja yenye nguvu mbele ya Serikali, ni lazima kijana wa kijijini awe na fursa sawa ya kueleza changamoto zake kama kijana wa mjini.
“Jukwaa hili halipaswi kubaki ngazi ya Taifa pekee. Ni lazima lishuke hadi ngazi ya jamii, likawafikie vijana kule vijijini ili wote wawe na sauti moja katika kueleza shida zao na matarajio yao kwa Serikali,” aliongeza.
Waziri Nanauka aliongeza kuwa kupitia jukwaa hili, vijana watapata fursa ya kubaini fursa za kiuchumi ambazo hazitumiwi kikamilifu, ikiwemo mgawo wa ekari 170,000 za ardhi zilizotengwa kwa ajili ya kilimo na viwanda. Aliwataka vijana kutumia nafasi hiyo kwa uzalendo na uadilifu, akisisitiza kuwa Serikali itatumia maoni yao kuboresha mifumo ya utendaji nchini.
Amani ndio Mtaji wa Machinga na Vijana
Wakati Serikali ikifungua milango ya fursa, wadau wa biashara ndogondogo (Machinga) wamepongeza juhudi hizo wakikumbusha kuwa mafanikio yoyote yanategemea uwepo wa amani na utulivu. Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Mkoa wa Pwani, Filemon Maliga, amesema amani ndiyo kila kitu kwa mfanyabiashara kwani hata wawekezaji huangalia utulivu wa sehemu kabla ya kuwekeza.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Joyce Mramba, mfanyabiashara wa Soko la Michonjo, Uyaoni Kibaha, aliyeeleza kuwa bila amani shughuli za kila siku za kutafuta riziki zitasimama. Alitoa mwito kwa Watanzania kuiombea nchi utulivu ili mshikamano wa kitaifa uendelee kudumu.
Naye Mwenyekiti wa Soko la Michonjo, Iddi Bundala, alionya kuwa kuvunjika kwa amani kuna athari za moja kwa moja kwenye uchumi wa kijana mmoja mmoja, hususan wale wenye mikopo. Alisema kuwa bila utulivu, marejesho ya mikopo hayawezekani, hivyo akawataka vijana kujiepusha na makundi yanayoweza kusababisha machafuko.
Maendeleo ya Kidijiti na Maeneo ya Vijijini
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Jenifa Omolo, alifafanua kuwa jukwaa hilo limeundwa kuwafikia vijana kuanzia ngazi ya jamii hadi Taifa kwa kutumia mifumo ya kidijiti. Alisema lengo ni kuziba pengo la mawasiliano kati ya vijana, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kijana wa kijijini na mjini anapata haki na fursa sawa katika ujenzi wa Taifa.
Uzinduzi huu unaweka historia mpya ambapo sauti ya kijana sasa inapewa thamani ya kitaalamu na kisheria, huku ikisisitizwa kuwa amani ndiyo mhimili utakaowezesha Jukwaa la Vijana kufikia malengo yake ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi nchini Tanzania.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464