Na OWM - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemuelekeza Mkandarasi MCB Company LTD, Mbeya University of Science and Technology kukamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ifikapo Julai 2026.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Januari 17, 2026 mjini Morogoro, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo ambapo alianza ukaguzi wa mradi huo wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, ambao ulianza kutekelezwa rasmi Mei 27, 2022 na ulitakiwa kukamilika Mei 26, 2024.
“Ninaelekeza mwezi Julai jengo liwe limekamilika, kwani fedha ipo, Mshauri Elekezi ambaye ni Wakala wa Majengo upo na Mkandarasi upo,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Sanjari na hilo, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima kutomuongezea muda mkandarasi iwapo atashindwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, na kuelekeza atafutwe mkandarasi mwingine atakayekamilisha jengo hilo kwa wakati.
Prof. Shemdoe amemuhimiza Mshauri Elekezi TBA kuhakikisha anatekeleza wajibu wake kikamilifu na kuahidi kurejea mwezi Julai ili kujiridhisha iwapo maelekezo yake yametekelezwa, na kuongeza kuwa mwaka 2022 alishuhudia ujenzi wa msingi wa jengo hilo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akiwa ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Aidha, amemtaka Mshitiri ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa kukutana na Mshauri Elekezi TBA pamoja na Mkandarasi MCB Company Limited ili kuandaa mpango kazi wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kuuwasilisha kwake ndani ya wiki moja.
Kwa upande wake, Msanifu Majengo Bw. Justine Katabaro kutoka kampuni ya MCB Company Ltd iliyopewa kandarasi amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Prof. Shemdoe ya kukutana na mshitiri pamoja mshauri elekezi ili kuandaa mpango kazi utakaowezesha kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro na kulikabidhi mwezi Julai, 2026.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi, Mhandisi Khamadu Kitunzi kutoka TBA amesema jengo hilo ni la ghorofa tatu (3), ambapo sakafu ya chini imetengwa kwa ajili ya maegesho ya magari ya watu mashuhuri na ofisi ya madereva na sakafu ya kwanza na ya pili imetengwa kwa ajili ya ofisi za watumishi na ukumbi huku sakafu ya tatu ikitengwa kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa.






