` DIPLOMASIA YA MADINI NA UCHUMI: JIBU KWA WANAOTAKIA TANZANIA MIZOZO NA KUVAMIWA

DIPLOMASIA YA MADINI NA UCHUMI: JIBU KWA WANAOTAKIA TANZANIA MIZOZO NA KUVAMIWA

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na sauti za baadhi ya watu wasiolitakia mema taifa letu wakijaribu kupandikiza hofu na uvumi wa ajabu kuhusu usalama wa Tanzania huku wengine wakifikia hatua ya kuota ndoto za mchana kuhusu nchi kuvamiwa kijeshi. 

Hata hivyo ukweli wa mambo unazidi kuwaumbua wapandikiza chuki hao kwani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kupitia diplomasia ya kiuchumi na ushirikiano wa kibiashara na mataifa makubwa duniani ikiwemo Marekani. 

Jibu la wazi kwa wale wanaotamani kuona mizozo nchini limetolewa jijini Dodoma kupitia kikao kizito cha kikazi kilichowahusisha wataalamu wa Wizara ya Madini ya Tanzania na ujumbe maalum kutoka Ubalozi wa Marekani ambao unalenga kuimarisha utafiti wa kina wa madini ya kimkakati yakiwemo madini ya kinywe kwa ajili ya tija na ajira kwa Watanzania.

Hatua ya Serikali ya Marekani kuingia mkataba wa ushirikiano wa kiufundi kupitia programu maalumu ya usimamizi wa nishati na madini ni kielelezo tosha kuwa Tanzania inahitaji marafiki wa kibiashara na siyo mizozo ya kijeshi kama wanavyodai wapotoshaji. 

Marekani inatambua kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani chenye fursa lukuki za kiuchumi na ndiyo maana mwelekeo wa sasa ni kuimarisha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuzipatia teknolojia za kisasa. 

Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameweka wazi kuwa ushirikiano huu utasaidia kubaini na kuibua migodi mikubwa ya madini ya kinywe katika mikoa ya Mtwara na Lindi jambo ambalo litaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wakazi wa mikoa hiyo na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Ushirikiano huu wa kimkakati haujaja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa inayo kwa uongozi wa Rais Samia na mazingira tulivu ya uwekezaji yaliyopo nchini. 

Marekani ambayo imekuwa mshirika wa maendeleo kwa miongo kadhaa katika sekta za afya, elimu na miundombinu sasa inaelekeza nguvu kwenye sekta ya madini ambayo ni uti wa mgongo wa viwanda vya kisasa duniani. 

Badala ya kusikiliza sauti za watu wanaohamasisha vurugu kwenye mitandao ya kijamii wananchi wanapaswa kuona vitendo vya dhati vya serikali kutoa zana za kisasa kama vishikwambi na vifaa vya uchambuzi wa jiosayansi ambavyo vinaimarisha uwezo wa wataalamu wetu wa ndani. 

Hii ni Tanzania inayojengwa kwa mikataba ya kibiashara yenye tija na siyo nchi inayotishwa na hofu za kufikirika za uvamizi wa kijeshi ambazo hazina msingi wowote wa kiuhalisia.

Ukweli ni kwamba maadui wa maendeleo wameumbuka kwani dunia inaona namna Tanzania inavyosonga mbele kwa kasi katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii. 

Uwepo wa kaimu balozi wa Marekani Andrew Lentz jijini Dodoma akizungumzia fursa za utafiti wa madini ni dhihirisho kuwa uhusiano wetu na mataifa makubwa upo imara na unazidi kuchanua. 

Huu ni wakati wa Watanzania kupuuza propaganda za mivutano na badala yake kuelekeza nguvu katika kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwenye sekta bunifu na za uzalishaji kama madini na sanaa.

 Sera za uchumi na fedha zimeanza kuzaa matunda baada ya nchi kuondolewa kwenye orodha hatarishi na sasa milango ya uwekezaji imefunguliwa kwa kiwango kikubwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya taifa letu.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464