Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amefanya mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi, huku akiagiza kufanyika kwa msako wa kuwakamatwa waendeshaji wa bodaboda waliotoboa eksozi za pikipiki zao, kitendo kinachosababisha kelele na milipuko inayotishia afya na usalama wa wananchi, hususan wenye presha.
Mkutano huo umefanyika leo Januari 6, 2026, katika Viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, Mtatiro amesema utatuzi wa kero za wananchi kwa sasa unazingatia ushirikishwaji wa jamii, ndiyo maana Serikali imeamua kuandaa mikutano ya hadhara ili kusikiliza maoni, ushauri na changamoto zinazowakabili wananchi.
“Viongozi wa sasa ni kukaa na jamii, kupata ushauri, maoni na kusikiliza kero zao mbalimbali na kuzitatua na mikutano hii itakuwa endelevu katika kuhakiksha wananchi wanaishi kwa furaha kwenye nchi yao,”amesema Mtatiro.
Amewataka pia wananchi, kwamba siku ya kufungua shule Junuari 13, watoto wote wenye sifa ya kupelekwa shule wapelekwe na hataki kuanza kukimbizana na mzazi yoyote.
Katika hatua nyingine, Mtatiro aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani ya nchi, akiwataka kutokuyumbishwa na taarifa au propaganda kutoka kwa watu wachache kupitia mitandao ya kijamii.
“Tusikubali amani yetu kuyumbishwa. Tuendelee kuilinda kwa wivu mkubwa,” amesisitiza.
Akijibu kero za wananchi, Mtatiro aliagiza mara moja kuanza kwa msako wa kuwakamatwa vijana wa bodaboda waliotoboa eksozi za pikipiki zao, akieleza kuwa pikipiki hizo zitakamatwa kwa mujibu wa sheria.
Pia ameagiza, kero zote zilizowasilishwa katika mkutano huo kufanyiwa ufuatiliaji wa karibu, na wananchi kupewa mrejesho wa hatua zitakazochukuliwa katika kuzitatua.
Katika mkutano huo, wananchi waliwasilisha kero mbalimbali zikiwemo uchakavu wa miundombinu ya Soko la Nguzo Nane, migogoro ya ardhi, ubovu wa miundombinu ya barabara, utolewaji wa mikopo ya asilimia 10, kuongezeka kwa vibaka, tozo za kodi pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Bugayambelele.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akisikiliza kero za wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze akizungumza.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga Said Kitinga akizungumza.
Wananchi wakiwasilisha kero zao.
Wananchi wakiendelea kuwasilisha kero.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464