Na Johnson James, KISHAPU
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameongoza harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Msingi Mwamasololo, Kata ya Sekebugoro, Wilaya ya Kishapu, ambapo jumla ya shilingi milioni 38.6 zimepatikana kati ya milioni 38.6 zinazohitajika.
Harambee hiyo ilifanyika mara baada ya wananchi wa Kijiji cha Mwamasololo kuwasilisha kilio chao kuhusu kutokamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa, hali inayowalazimu watoto kusomea katika mazingira duni yasiyo rafiki kwa elimu bora.
Mara baada ya kusikia kero hiyo, RC Mhita aliamua kuchukua hatua ya haraka kwa kuendesha harambee papo hapo, na kufanikisha upatikanaji wa kiasi hicho cha fedha, hatua iliyowaletea faraja kubwa wananchi na wazazi wa eneo hilo.
“Nimekuja hapa kusikiliza na kutatua changamoto zenu. Sijisikii vizuri kuona watoto wetu wakisomea kwenye mazingira magumu ilhali tuna uwezo wa kuchangia na kuboresha hali hiyo. Tumechanga, tumeanza, na ujenzi utaendelea mara moja,” alisema RC Mhita mbele ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara.
Wananchi wa kijiji hicho walimpongeza RC Mhita kwa moyo wake wa kujitolea na kuchukua hatua za haraka, wakisema matumaini yao ya kupata madarasa mapya yalikuwa yamepotea lakini sasa yamefufuka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, aliahidi kusimamia kikamilifu ujenzi huo ili kuhakikisha madarasa yanakamilika kwa wakati na kuanza kutumika mapema iwezekanavyo.
Ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara moja na utagharimu jumla ya shilingi milioni 38.6, ambapo kiasi kilichobaki kinatarajiwa kukamilishwa kwa ushirikiano wa wadau na halmashauri.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464









