` DIAMOND AIPONGEZA JAB, AAHIDI VYOMBO VYAKE KUFUATA SHERIA YA HABARI

DIAMOND AIPONGEZA JAB, AAHIDI VYOMBO VYAKE KUFUATA SHERIA YA HABARI

Diamond aipongeza JAB, aahidi vyombo vyake kufuata Sheria ya Habari

Mkurugenzi wa Wasafi Media, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, ameipongeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, akiahidi kuwa vyombo vyake na watumishi wake wako tayari kuzingatia matakwa yote ya kisheria yanayohusu sekta ya habari.

Akizungumza baada ya kufika katika ofisi za JAB kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala ya kisheria, Diamond amesema Wasafi Media haina nia ya kukwepa utekelezaji wa Sheria, bali inalenga kushirikiana kikamilifu na wasimamizi wa taaluma hiyo ili kuimarisha weledi na nidhamu kwa waandishi wa habari.

Amesema licha ya Sheria ya Huduma za Habari kuathiri vyombo vya habari kwa namna moja au nyingine, ni Sheria halali iliyotoa muda wa kutosha kwa wadau kujipanga na kutimiza vigezo vilivyowekwa, ikiwemo waandishi kuwa na kiwango cha elimu cha angalau Diploma, hatua ambayo Wasafi Media imeanza kuitekeleza.

Diamond amekiri kuwa ujio wa Bodi ya Ithibati umeleta nidhamu na uwajibikaji mkubwa katika taaluma ya habari, akisisitiza kuwa Wasafi Media inaunga mkono juhudi za Serikali za kulinda maadili, weledi na heshima ya taaluma hiyo nchini.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema Sheria ya Huduma za Habari ilitungwa mwaka 2016 na ilitolewa kipindi cha mpito cha kutosha kwa waandishi na wadau wote kutimiza vigezo vya kisheria, kwa lengo la kujenga sekta ya habari yenye misingi imara, weledi na uwajibikaji.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464