Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetua mkoani Shinyanga kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji wa ndani na kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu rafiki kwa wawekezaji.
Akizungumza leo Januari 29, 2026, Meneja wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani kutoka TISEZA, Felix John, amesema ziara hiyo imelenga kukagua na kubaini hali ya uwekezaji pamoja na changamoto zinazoweza kuwakabili wawekezaji, hususan katika sekta ya elimu.
John ameyasema hayo mara baada ya kufanya ukaguzi wa uwekezaji katika Shule ya Msingi na Sekondari Savannah, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kwa kuboresha miundombinu muhimu kama maji, umeme, barabara na mawasiliano katika maeneo yote ya uwekezaji,” amesema John.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Wema Kanika, amesema uwekezaji uliofanyika shuleni hapo unanufaisha wanafunzi 936 kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.
“Shule imejengwa katika eneo la hekta 80, ikiwa na wanafunzi 512 wa elimu ya awali na msingi pamoja na wanafunzi 424 wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Pia tuna wafanyakazi 50 wanaoishi ndani ya shule,” amesema Wema.
Ameongeza kuwa shule hiyo pia imewekeza katika ufugaji wa ng’ombe kwa ajili ya nyama na maziwa ya wanafunzi, visima vya maji pamoja na upandaji wa miti ya matunda.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema mkoa huo umetenga maeneo mawili makubwa kwa ajili ya uwekezaji wa kiuchumi ambayo ni Buzwagi na Nyanshimbi.
“Hakuna eneo la uwekezaji katika mkoa wa Shinyanga lisilo na miundombinu ya uwezeshaji. Aidha, uwepo wa bandari kavu utaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huu,” amesema Mhita.
Viongozi kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) wakitembelea shule ya msingi Savanah




