Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imeendesha mafunzo kwa walipakodi mkoani humo, kuhusu mfumo mpya wa kielektroniki wa usimamizi na ukusanyaji wa kodi za ndani ‘IDRAS,’ ili kuboresha utoaji wa huduma, ambapo mlipakodi atajihudumia mwenyewe kupitia mtandaoni ‘online’.
Mfumo huo wa IDRAS (Integrated Domestic Revenue Administration System), utaunganishwa pia na akili unde, ili kumsaidia mlipa kodi kuuliza maswali na kupata majibu papo hapo, bila hata ya kufika TRA.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo leo Januari 27,2026 Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Maro, amesema mfumo huo wa IDRAS, utasaidia kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi, uelewa, kuboresha utunzaji wa kumbukumbu, kuongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma saa 24, kupunguza malalamiko ya mashine ya EFD , kupunguza adhabu na migogoro isiyo ya lazima, pamoja na na kuchochea ulipaji kodi kwa hiari.
“Mafunzo haya tumeamua kuyatoa mapema kwa walipa kodi wetu hapa Shinyanga, sababu ifikapo Februari 9 mwaka huu, mfumo huu utaanza kutumika rasmi kwa kila kitu kufanyika mtandaoni ‘online’, amesema Maro.
Ameongeza kuwa, mfumo huo umekuja kuchukua nafasi ya mifumo mbalimbali iliyokuwa ikitumika awali ndani ya TRA, kwa lengo la kupunguza matumizi ya makaratasi na kuhamishia huduma zote za kodi katika mfumo wa kidijitali.
Amefafanua kuwa kupitia mfumo huo, walipakodi wataweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo usajili na uboreshaji wa taarifa zao, uwasilishaji wa matamko ya kodi, makadirio na utozaji wa kodi, malipo ya kodi kwa njia za kielektroniki, ufuatiliaji wa madeni, maombi ya marejesho ya kodi, mapingamizi ya maamuzi ya kikodi pamoja na maombi ya misamaha ya riba na adhabu.
Aidha, amesema mfumo huo utawezesha pia utoaji wa huduma za leseni mbalimbali ikiwemo leseni za udereva na leseni za uzalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa, pamoja na utoaji wa hati za uthibitisho wa ulipaji kodi (Tax Clearance) moja kwa moja kwa walipakodi wanaostahili.
Katika kuimarisha uwazi na uaminifu, mfumo wa IDRAS utawezesha uthibitishaji wa nyaraka za kodi kwa kutumia misimbo ya QR (QR Codes), pamoja na kuwapa walipakodi uwezo wa kuona historia na kumbukumbu zao zote za ulipaji kodi.
Ameeleza kuwa mfumo huo umeunganishwa na mifumo mingine ya taasisi za umma na binafsi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mifumo ya taasisi mbalimbali inawasiliana ili kuboresha utoaji wa huduma. katika siku zijazo, IDRAS unatarajiwa kuunganishwa na mifumo ya malipo (billing systems), mishahara (payroll systems) na uhasibu.
Maro amewahimiza walipakodi kutumia kikamilifu kipindi cha mpito (Pre-Launch) kilichowekwa na TRA kabla ya kuanza rasmi kwa mfumo huo, ikiwemo kuhakiki taarifa zao, kupata nywila na kuthibitisha au kuteua wawakilishi wao wa kikodi.
Pia amewakumbusha walipakodi kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kisheria ikiwemo uwasilishaji wa ritani za makadirio ya kodi ya mapato kwa mwaka 2026, huku akiwataka kushirikiana na mamlaka hiyo ili kuhakikisha mafanikio ya utekelezaji wa mfumo mpya wa IDRAS.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema, mfumo huo mpya, utasaidia kupata huduma kwa wakati pamoja na kutipoteza muda kwenda kwenye Ofisi za TRA bali huduma zote watazipata kupitia mtandao.
TAZAMA PICHA👇👇
Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga Emmanuel Maro akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo ya IDRAS yakiendelea kwa walipa kodi mkoani Shinyanga.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464