Na Marco Maduhu, SHINYANGA
WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga, umekabidhi pikipiki tano kwa vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSO, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Makabidhiano ya pikipiki hizo yamefanyika leo Januari 22, 2026 katika Ofisi za RUWASA Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, John Singolile, amewataka viongozi wa CBWSO kuzitumia pikipiki hizo kwa madhumuni yaliyokusudiwa, ili kuongeza ufanisi wa utendaji wao na kutatua changamoto za huduma ya maji kwa wakati.
Amesema pikipiki hizo lengo lake ni kuwawezesha watoa huduma hao kufika kwa haraka katika maeneo yenye changamoto za maji, ikiwamo kufanya matengenezo ya miundombinu na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa wakati.
“Lengo la pikipiki hizi ni kuboresha utendaji wenu kazi, na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati, na mzitumie kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili ziwe na tija,” amesema Singolile.
Kwa upande wake, Afisa Manunuzi wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Edmond Kanonika, amesema pikipiki hizo zenye thamani ya sh. milioni 14.6 zimekabidhiwa kwa CBWSO nne, ambapo CBWSO ya Songambele imepewa pikipiki mbili, huku CBWSO za Mahembe, Solwa na Bulyanhuru zikipewa pikipiki moja moja.
Naye mmoja wa viongozi wa CBWSO, Monica Francis, amesema pikipiki hizo zitawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, na kuboresha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi, ikilinganishwa na hapo awali, ambapo walikuwa wakitumia usafiri wa baiskeli.
TAZAMA PICHA👇👇
Kaimu Mweneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga John Singolile akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464