Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amewataka viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya afya na madiwani, kutumia mikutano yao na vikao mbalimbali, kuwahamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote, ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi pale wanapokumbwa na changamoto za kiafya.
Mhita ametoa wito huo leo Januari 16, 2026, wakati akifungua kikao cha tathimini ya mkataba wa lishe, na utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, kilichowakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya afya mkoani humo.
Amesema mpango wa bima ya afya kwa wote ni dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za afya kwa usawa bila kujali hali zao za kiuchumi, na hivyo kuwataka wananchi kujiunga na bima hiyo ili kujihakikishia upatikanaji wa matibabu kwa wakati hasa pale watakapopata changamoto za kiafya za kukutwa hawana pesa za matibabu.
“Leo yanatolewa mafunzo ya bima ya afya kwa wote kwa viongozi mbalimbali wakiwamo madiwani, lengo ni kuhakikisha mnaenda kuwahamasisha wananchi kupitia mikutano yenu na kuwapatia elimu ili wajiunge na bima ya afya, jambo litakalowapunguzia gharama za matibabu na kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi na usawa,” amesema Mhita.
Ameongeza kuwa ugonjwa haupigi hodi na hakuna mtu aliye na uhakika wa kuwa salama kiafya wakati wote, hivyo kuwa na bima ya afya kunawapunguzia wananchi hofu ya gharama za matibabu wanapokosa fedha.
“Mtu akiwa na bima ya afya kwa wote hatakuwa na wasiwasi anapopata changamoto ya kiafya, kwa sababu atapata huduma hata kama hana fedha,” ameongeza.
Aidha, Mhita amesema serikali imeweka utaratibu maalumu wa kuzikatia bima kaya zisizo na uwezo wa kifedha, ambapo kaya hizo zitatambuliwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu kwa Umma wa Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya Said Makora, amesema kuwa Bunge lilipitisha sheria ya bima ya afya kwa wote mwaka 2023, huku Wizara ya Afya ikitunga kanuni za utekelezaji Agosti 2024.
Makora amesema, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo, utaanza kwa kuwalenga makundi maalumu yasiyo na uwezo wa kifedha, akibainisha kuwa faida kubwa ya bima ya afya kwa wote ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa usawa kwa wananchi wote.
Naye Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Shinyanga Isaac Katenda, amesema kifurushi cha bima ya afya kwa kaya yenye watu sita ni Shilingi 150,000 kwa mwaka, ambapo wanufaika hupata huduma za matibabu kwa kipindi chote cha mwaka.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wameahidi kwenda kutoa elimu na hamasa kwa wananchi katika maeneo yao ili kujiunga na bima ya afya kwa wote, wakisema mpango huo ni mkombozi kwa wananchi wenye kipato cha chini.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza kwenye kikao hicho.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Shinyanga, Isaac Katenda, akizungumza kwenye kikao hicho.
Meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Magharibi Awanje Matenda akiwasilisha wasilisho la TIRA.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464