RC MBONI AKAGUA MIRADI YA BILIONI 27 MANISPAA YA SHINYANGA
Na; Richard Bagolele - SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita amefanya ziara katika Manispaa ya Shinyanga na Kuzindua, kuweka jiwe la Msingi na kutembelea miradi katika kata tatu yenye jumla ya Shilingi Bilioni 27.
Akizindua mradi wa kituo cha Afya Ihapa kilichopo kata ya Old Shinyanga, Mhe. Mhita amepogeza kwa ujenzi wa Kituo hicho ambapo amesema litakuwa mkombozi kwa wananchi hao kwani kituo hicho kinatoa huduma zote za Matibabu na kina vifaa tiba vya kisasa pamoja na watoa huduma wenye sifa hivyo amewataka wakitunze.
"Nataka nimshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea Kituo hiki cha Afya kizuri ambacho kinakwenda kuwa mkombozi katika eneo hili. Niwasihi wananchi tujenge tabia ya kupima Afya zetu mara kwa mara kwani huduma sasa zimesogezwa karibu yenu wananchi" amesema Mhe. Mhita.
Mhe. Mhita ameongeza kusema kuwa katika miradi iliyokagua Serikali imetoa fedha nyingi katika Mkoa hususan Manispaa ya shinyanga hivyo amewataka wananchi kukilinda na kuithamini miradi hiyo kwani inakwenda kutatua matatizo mengi katika kila sekta pia amepongeza uongozi wa Manispaa kwa usimamizi nzuri wa miradi hiyo ambapo amewata mafundi na wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuongeza kasi ya ukamilishaji wa miradi hiyo.
Miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na uwekaji wa jiwe la Msingi la shule mpya ya awali na Msingi ya Butulwa kupitia mradi wa BOOST wenye jumla ya Shilingi 342,900,00 pamoja na mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya miji nchini (TACTIC) ambapo unahusisha ujenzi wa Barabara za lami mjini Shinyanga zenye urefu wa kilometa 6, Ujenzi wa Kituo kipya cha Mabasi kilichopo Kata ya Kizumbi na ujenzi wa ofisi ya Wahandisi ambayo inatekelezwa na Kampuni ya SIHOTECH Engineering Company kwa gharama ya Shilingi Bilioni 26.5 kwa muda wa miezi 15.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464










