Mwaka 2026 umeanza kwa kishindo, huku sauti za Watanzania wa kada mbalimbali zikijielekeza katika jambo moja kuu, Amani kama mhimili wa maendeleo.Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, ameweka wazi kuwa bila amani, sekta nyeti kama utalii haziwezi kustawi. Kauli hii inaungwa mkono na Hussein Hassan (Mkufunzi MUM), anayekumbusha kuwa amani ndiyo inayotoa uhuru wa kuabudu na kusoma.
Kwa upande wake, Athumani Saidi kutoka Mwanga, anabainisha kuwa uzalendo wa kweli unazaliwa pale tu nchi inapokuwa na utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Hofu ya vurugu imetajwa kuwa tishio kwa makundi yenye uhitaji. Husna Tauka wa Mikumi na Victoria Mkwizu wa Iringa, kwa nyakati tofauti, wameonya kuwa machafuko huwaumiza zaidi wanawake, watoto, wazee, na watu wenye ulemavu.
Hali hii inamfanya Mary Makoa wa Morogoro kutoa wito kwa vijana kutoruhusu kuchochewa kuasi na kufanya vurugu, ili warithi taifa lenye amani ambalo waasisi walilijenga kwa miaka mingi.
Pamoja na sauti hizo za wananchi, mwaka 2026 unatajwa kuwa mwaka wa "Siasa za Busara" huku kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana kukiwa ni kiashiria tosha kuwa sauti za vijana sasa zinapaswa kuwa sehemu ya maamuzi na si kelele za pembezoni.
Uchambuzi wa mwelekeo wa sasa unaonyesha kuwa Taifa linahitaji kuachana na siasa za kejeli na matusi ambazo huwafanya vijana kuamini kuwa siasa ni uwanja wa visasi. Maridhiano ya Rais Samia yanapaswa kuwa sera na utamaduni, si hotuba pekee ili amani inayozungumzwa na akina Victoria Mkwizu na Mary Makoa iwe ya kudumu.