
Sauti za wananchi na wajasiriamali nchini zimeendelea kupazwa zikimtaka Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kusimamia sheria kwa ukamilifu na kutoonesha huruma kwa watu wanaopanga kuvuruga amani, kuhujumu miundombinu, na kuhatarisha uhuru wa nchi (Sovereignty).
Uhalifu Siyo Haki ya Kikatiba
Katika mjadala unaoendelea nchini, imebainika kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kudai haki na kufanya uhalifu. Wananchi wameonya kuwa wasiwasi wa "kusamehewa mara kwa mara" kwa wachochezi unawafanya wahalifu hao "kuvimba vichwa" na kuendelea kupanga njama za kuleta machafuko.
"Maandamano ya vurugu ni uhalifu, na wahalifu hawapaswi kuonewa huruma. Ukionyesha huruma mahali pasipostahili, unakaribisha vifo, uharibifu wa mali, na dharau dhidi ya mamlaka ya nchi," amesema mmoja wa wadau wa usalama jijini Dar es Salaam.
Kukataa Kuingiliwa na Mataifa ya Nje kupitia 'Manywele'
Katika kile kinachoonekana kama kukataa mbinu za kurubuniwa, Watanzania wamemtaja Maria Sarungi (Manywele) kama mmoja wa watu wanaopaswa kupuuzwa. Wananchi wamesisitiza kuwa ni wakati wa "kuzungumza ya kwetu" kwa amani na kutumia Tume zilizopo kutatua migogoro badala ya kufuata maelekezo ya watu walioko nje ya nchi ambao hawaguswi na machafuko yakitokea.
Wananchi wamemtaka Amiri Jeshi Mkuu Kupitia jumbe mbalimbali, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ulinzi wa mamlaka ya nchi unaendelea. wamemtaka kuhakikisha analinda mipaka na utulivu wa ndani dhidi ya mamlaka yoyote ya nje inayojaribu kutumia mawakala wa ndani kuvuruga nchi.
Aidha wamevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi yake kwa mujibu wa sheria. "Huruma isiyofuata sheria ni malezi mabaya yanayoweza kuliingiza taifa kwenye giza," ilieleza sehemu ya tamko la wajasiriamali.
Wakirejea hujuma za hivi karibuni (kama ilivyotokea Hospitali ya Temeke kuhusu x-ray ), wananchi wamesema kuwa kuharibu miundombinu ya serikali ni kumkomoa mwananchi mnyonge na si viongozi.
Watanzania wametakiwa kuwa wazalendo na kutokubali kuwa wasaliti wa nchi yao. Migogoro yote inaweza na inapaswa kutatuliwa kupitia meza ya mazungumzo na maridhiano yanayolenga kulisogeza taifa mbele, na si kurudi nyuma kwenye machafuko.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464