
Wakati Dunia ikikimbilia kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, Tanzania imechagua njia ya kipekee: Kugeuza viganja vya vijana wake kuwa viwanda vya teknolojia badala ya kuwa vyanzo vya malalamiko.
Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mezani mwarobaini wa kudumu wa changamoto ya ajira kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA).
Uamuzi wa kuanzisha "Open Coding Schools" na kufufua vituo vya kimkakati kama Ilonga na Sasanda, siyo tu mpango wa elimu, bali ni mkakati wa kiusalama na kiuchumi kuelekea Dira ya Maendeleo 2050. Huu ni ujumbe wa wazi kwa vijana: Zama za kusubiri bahasha za bahati zimepita; sasa ni zama za kuandika misimbo (Coding) inayotatua matatizo ya jamii.
Coding: Zaidi ya Teknolojia, ni Uhuru wa Kiuchumi
Fikiria kijana anayetumia saa tano mtandaoni. Je, anatumia muda huo kupokea maelekezo ya "wanaharakati waovu" wanaolenga kuchoma moto nchi yake na kubomoa amani? Au anatumia muda huo kusoma Python, Java, au Mobile App Development?
Coding inampa kijana uwezo wa kutengeneza mifumo inayounganisha mkulima wa kijijini na masoko ya kidunia. Inamfanya kijana wa Songwe au Kilimanjaro kutengeneza suluhisho (Apps) za kukodisha vifaa vya ujenzi au kusimamia mifumo ya afya. Hapa, kijana hahitaji 'connection' ya kujuana na mtu; anahitaji akili, kompyuta, na utulivu wa nchi.
Amani Ndiyo 'Server' ya Maendeleo
Wataalamu wa usalama na uchumi wanabainisha kuwa bila amani, hakuna intaneti, hakuna utalii, na hakuna mikopo ya asilimia 10. Kijana anayejitambua hawezi kukubali kutumika kama 'kiberiti' cha kuwasha moto nchi yake. Akijua kuwa amani ikivurugika, mnyororo mzima wa uchumi unakatika—kuanzia kwa Mama Lishe anayepoteza wateja hadi kwa mtaalamu wa Coding anayepoteza soko la kimataifa.
Kama alivyowahi kunukuliwa Askofu Dkt. George Pindua, "Tupambane na chochote kinachotishia misingi yetu ya umoja." Uzalendo wa karne ya 21 ni kulinda taswira ya Tanzania mtandaoni na kuitumia teknolojia kukuza pato la taifa, badala ya kuwa mshabiki wa propaganda zinazofadhiliwa na washindani wa taifa letu.
Nafasi ya Uwekezaji na Fursa Mezani
Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha TEHAMA (ICT Hub) Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa sasa, bilioni za shilingi ziko mezani kupitia mikopo na mifuko ya ubunifu (Innovation Funds). Kituo cha TEHAMA (ICTC) kinatoa fursa kwa vijana kugeuza mawazo (Startups) kuwa mamilioni ya dola.
Kwa nini uwekeze kwenye Coding sasa? La kwanza kabisa kuna soko la uhakika: Mahitaji ya mifumo ya kidijitali yanazidi kukua kila uchao.Pili kujiajiri: Unakuwa bosi wa akili yako na muda wako na tatu kulinda Taifa: Unatumia teknolojia kuelezea vivutio vya utalii na fahari ya Tanzania, ukishinda propaganda za maadui.
Wito kwa Kijana wa Kitanzania
Dira ya 2050 haitatimizwa na miujiza, bali na vijana wanaoamua kuwa sehemu ya suluhisho. Badala ya kutumika kama chombo cha chuki mtandaoni, geuza simu yako kuwa darasa. Ingia kwenye "Open Coding Schools", jifunze uandishi wa programu, na uwe Bill Gates ajaye wa Kitanzania.
Umaskini si kisingizio tena kama una uwezo wa kupata mtandao. Tumia amani iliyopo, tumia mikopo ya serikali, na tumia Coding ili kuyapatia maisha yako. Tanzania yenye uchumi wa kidijitali inaanza na msimbo (code) mmoja utakaoandika leo!
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464