` SIMBA WA SAANANE: MIAKA 10 YA UTAWALA, HADHI NA KIVUTIO KISICHOISHA

SIMBA WA SAANANE: MIAKA 10 YA UTAWALA, HADHI NA KIVUTIO KISICHOISHA


Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George akizungumza na waandishi wa habari

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane imeandaa tukio la kihistoria na la aina yake litakalowapa watalii na wananchi burudani ya kipekee, baada ya kutangaza kusherehekea miaka 10 ya simba anayeishi katika hifadhi hiyo. 

 Tukio hilo la kihistoria, ambalo halijawahi kufanyika katika hifadhi yoyote Tanzania, limepangwa kufanyika Desemba 20, 2025 katika kisiwa hicho kilichopo katikati ya Ziwa Victoria, jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 1, 2025, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, amesema sherehe hiyo itafanyika chini ya kauli mbiu “Saanane King Turns Ten” na itahusisha matukio ya aina yake yanayolenga kuhamasisha utalii na kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa wanyamapori.

“Simba ni mfalme wa nyika na mmoja wa wanyama maarufu barani Afrika na duniani. Katika Hifadhi ya Saanane, mnyama huyu amekuwa kivutio kikubwa na sehemu muhimu ya historia ya hifadhi. Tumetenga siku maalum kwa ajili yake ili kuenzi mchango wake katika utalii na elimu ya uhifadhi,” amesema Dkt. Tutindaga.
Dkt. Tutindaga amefafanua kuwa, wageni watapata nafasi ya kumuona simba huyo akilishwa keki maalum iliyotengenezwa kwa umbo na malighafi salama kwa mnyama huyo, pamoja na kusimuliwa historia yake, mwenendo wa maisha yake, tabia zake, na nafasi yake katika kundi maarufu la The Big Five.

Dkt. Tutindaga ameeleza kuwa tukio hilo linalenga si tu kuwaburudisha watalii, bali pia kuongeza thamani ya utalii wa mijini (urban tourism) katika Mkoa wa Mwanza na kuonyesha kwamba vivutio vya kipekee havipo tu katika hifadhi kubwa, bali pia katika hifadhi ndogo zilizo karibu na miji.

“Watalii wengi wanaokuja Saanane hupenda kusikia simulizi za maisha ya simba, familia yake, uwezo wake wa kuwinda, na hata tabia zake wakati wa honeymoon. Hivyo tukio hili litatoa elimu kwa kina kuhusu maisha ya mnyama huyu,” ameongeza.

Elimu, Zawadi na Maonesho kwa Wageni

Sherehe hiyo pia imelenga kuwanufaisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari, vyuo pamoja na makundi mengine ya jamii. 

Wageni hasa wanafunzi watapata nafasi ya kuulizwa maswali kuhusu uhifadhi ambapo washindi watapewa zawadi mbalimbali ikiwemo mabegi yenye picha ya simba na nembo ya Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.

Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Pellagy Marandu, amesema maandalizi yanaenda vizuri na kwamba siku hiyo itajumuisha maonesho ya uhifadhi, burudani, elimu kwa wageni na mawasilisho ya kihistoria kuhusu maisha ya simba huyo.
Pellagy Marandu

“Tumepanga siku ya burudani, elimu na ubunifu. Tunataka kila anayekanyaga Saanane tarehe hiyo ajue kuwa uhifadhi si nadharia tu, ni maisha halisi ya wanyama tunaoishi nao,” amesema.

Mkutano wa kutangaza tukio hilo umehudhuriwa pia na Anifa John (Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Wanyamapori), Andrea Idrissa Mbwambo (Daktari Msaidizi wa Wanyamapori) na Mwalimu Gilbert Tindabatangile kutoka Shule ya Sekondari Mkolani, jijini Mwanza.

Kwa sasa, simba anaendelea kubaki miongoni mwa wanyamapori maarufu zaidi duniani, akivutia watalii kwa ujasiri, nguvu na hadhi yake kama mfalme wa pori. 

Tukio hili linatarajiwa kuongeza hamasa, ubunifu na upekee katika utalii wa ndani, huku likiipa Saanane nafasi ya kipekee katika ramani ya vivutio vya kipekee barani Afrika.
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni moja ya maeneo adimu yanayosimamiwa na TANAPA, ikiwa na hadhi ya pekee kama hifadhi ya kwanza Tanzania iliyopo katikati ya mji. Iko umbali wa dakika 10 tu kwa boti kutoka katikati ya jiji la Mwanza, jambo linaloifanya kuwa kivutio rahisi na cha kipekee kwa watalii wa ndani na nje.

Kisiwa hiki kina eneo la takriban 2.18 km², hivyo ni hifadhi ndogo kuliko zote nchini, lakini pamoja na ukubwa wake, kina utajiri mkubwa wa viumbe na mandhari. Historia yake inaanzia mwaka 1964 kilipoanzishwa kama bustani ya wanyamapori, baadaye kuwa game reserve mwaka 1991, na hatimaye kuwa Hifadhi ya Taifa mwaka 2013 chini ya TANAPA.

Saanane ina mandhari maridadi yenye miamba ya graniti, maporomoko madogo, mwambao wa ziwa, misitu midogo na uoto wa porini unaowavutia wapenzi wa bird watching na watalii wanaopenda utulivu. Wanyama kama impala,simba, nyani, rock hyrax na ndege wa aina mbalimbali wanaonekana kwa urahisi.

TANAPA pia inaendeleza ubunifu wa utalii kupitia uanzishwaji wa mahema ya kulala (tented lodge) ndani ya hifadhi, hatua inayolenga kuifanya Saanane isiwe tu safari ya siku moja bali eneo la kukaa na kupata uzoefu kamili wa utalii wa mijini na pori kwa wakati mmoja.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464