` KIBURI CHA SWEDEN NA JIBU LA KISHUJAA:BALOZI MATINYI ALIVYOZIKA DHANA YA "TANZANIA MASIKINI"

KIBURI CHA SWEDEN NA JIBU LA KISHUJAA:BALOZI MATINYI ALIVYOZIKA DHANA YA "TANZANIA MASIKINI"

Na Mwandishi Wetu

Kwa miongo mingi, mataifa ya Magharibi yamejenga mazoea ya kuinyoshea kidole Tanzania kama nchi inayostahili huruma na misaada pekee. Lakini hivi karibuni, Waziri wa Sweden, Benjamin Dousa, alipojaribu kuitumia lugha hiyo ya kibeberu, aligonga mwamba wa takwimu na hoja nzito kutoka kwa Balozi wetu, Mhe. Mobhare Matinyi.

Waziri Dousa alidai Tanzania "imekwama kwenye Ujamaa" na "haina maendeleo." Hapa ndipo Balozi Matinyi alipoamua kuvua glavu. Kupitia gazeti hilo hilo la Aftonbladet, Matinyi ameiambia dunia kuwa Tanzania si ile ya mwaka 1961.

Balozi Matinyi hakujibu kwa hasira, alijibu kwa hekima na namba. Aliwakumbusha Waswidi kuwa wakati wao wana vyuo vikuu 18, Tanzania sasa ina vyuo 36. Wakati wao wakidhani tunasubiri misaada yao ya SEK milioni 560 (dola milioni 60), Tanzania inakusanya zaidi ya Dola Bilioni 4 kupitia dhahabu pekee!

Huu ni ujumbe kwa dunia: Tanzania sasa inatafuta Wafanyabiashara, siyo Wafadhili. Tunajenga Reli ya Kisasa (SGR), tuna mradi wa Gesi wa Dola Bilioni 42, na uchumi wetu unakua kwa kasi kuliko wa kwao. Jibu la Matinyi si tu utetezi wa kidiplomasia, bali ni tangazo la Uhuru wa Kiuchumi.

Ni wakati wa watanzania kujivunia hatua tuliyopiga. Kama Balozi wetu alivyosema, kuitaja Tanzania kama nchi isiyo na maendeleo ni "upotoshaji wa kusikitisha." Tanzania imepaa, na aliyelala bado anadhani tuko gizani.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464