
Wakati dunia ikitazama wapi pa kwenda kupata utulivu na vivutio vya kipekee, staa wa muziki na mfanyabiashara mkubwa duniani kutoka Marekani, Kanye West, ameweka wazi kuwa ndoto yake namba moja ni kuja Tanzania kuupanda Mlima Kilimanjaro. Hii siyo bahati mbaya; ni ishara ya imani ambayo watu mashuhuri duniani wanayo kwa nchi yetu.
Kwa hakika hii ni habari kubwa na ya kimkakati sana kwa taifa letu. Kanye West siyo tu msanii, bali ni "brand" ya kimataifa yenye wafuasi mamilioni duniani kote. Kitendo cha yeye kuweka Mlima Kilimanjaro kama kipaumbele chake namba moja (Number 1 Bucket List) ni tangazo la bure lenye thamani ya mabilioni kwa utalii wa Tanzania.
Kwa nini Kanye West anaitaka Tanzania? Jibu ni rahisi: Amani. Utalii hauwezi kukua pasipokuwa na amani. Watu wanakuja Tanzania kwa sababu wanajua ni nchi ya ukarimu, utulivu, na usalama. Mmarekani huyu anauota mlima wetu kwa sababu anajua Tanzania ni "Kisiwa cha Amani" katikati ya misukosuko ya dunia.

Kutokana na ukweli huu tunapaswa kuwashinda wanaotutia doa. Kuna wachache wanaotumia nguvu zao kutafuta manufaa binafsi kwa kujaribu kuipaka rangi nchi yetu na kutafuta kutuvuruga. Lakini ukweli unabaki palepale: Sisi tuko wengi, na wao ni wachache.
Sisi tunaopenda amani, mshikamano, na maendeleo ndio wenye nchi hii. Tusiwaruhusu watu wachache wenye njaa ya madaraka au maslahi binafsi watuharibie "brandi" ya nchi yetu ambayo sasa hata mastaa wakubwa duniani wanaipigania kuja kuiona.
Tanzania ni Taifa Kubwa Kanye West kutaka kuja hapa ni fursa ya kiuchumi. Itavutia wawekezaji, itatengeneza ajira kwa vijana wetu (wapanda milima, mahoteli, na madereva), na kuitangaza Tanzania zaidi kijiopolitika. Sisi ni Taifa kubwa lenye rasilimali nyingi, na kubwa kuliko zote ni Amani yetu.
Swali kwa Watanzania: Mmarekani anatamani kuja kwetu kuona fahari yetu, wewe Mtanzania unajivunia vipi rasilimali zako? Je, una mpango gani wa kutembelea vivutio vyetu na kulinda amani inayovivuta hivi viumbe vikubwa duniani kuja kwetu?
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464