
Katika ulimwengu wa sasa ambapo teknolojia ya mawasiliano imekua kwa kasi, simu janja mkononi mwa kijana imekuwa silaha yenye nguvu inayoweza kujenga mustakabali wa nchi au kubomoa misingi ya amani iliyodumu kwa miongo mingi.
Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikihimiza uhuru wa kutoa maoni kama haki ya kikatiba, kumeibuka changamoto ya baadhi ya vijana kutumbukia kwenye makosa ya jinai kupitia mitandao ya kijamii, ama kwa kufuata mikumbo ya kisiasa au kwa kukosa uelewa wa mipaka ya kisheria.
Ili kulinda usalama wa taifa na mustakabali wa vijana wenyewe, kuna haja ya kuwa na uelewa wa kina juu ya maadili ya kidijitali yanayozingatia uzalendo na utii wa sheria.
Msingi wa kwanza wa kuwa raia mwema wa kidijitali unaanza na dhana ya kuhakiki taarifa kabla ya kuzisambaza. Katika mazingira ya sasa ambapo taarifa za uongo au "Fake News" husambaa kwa kasi ya ajabu, ni wajibu wa kila kijana kujiuliza juu ya ukweli wa jambo kabla ya kubofya kitufe cha kusambaza.
Sheria ya Makosa ya Mtandao iko wazi kuwa kusambaza taarifa ambazo mtu anajua au anapaswa kujua kuwa ni za uongo na zinaweza kuleta taharuki nchini ni kosa la jinai. Badala ya kuwa sehemu ya kusambaza uzushi kuhusu usalama wa taifa au afya za viongozi, kijana mzalendo anapaswa kusubiri taarifa kutoka kwenye vyanzo rasmi vya serikali na vyombo vya habari vinavyotambulika.
Hali kadhalika, kuna tofauti kubwa kisheria kati ya kukosoa utendaji wa serikali na kutoa lugha za kashfa au kejeli dhidi ya viongozi na mamlaka halali. Kukosoa sera au mipango ya maendeleo kwa lengo la kuleta maboresho ni sehemu ya ujenzi wa taifa na ni haki inayolindwa.
Hata hivyo, kutumia lugha za matusi, kudhalilisha utu wa mtu, au kutoa lugha za kashfa dhidi ya Rais na viongozi wengine ni ukiukwaji wa maadili na uvunjifu wa sheria.
Kijana anayejitambua anapaswa kujikita kwenye hoja zenye mashiko (issues) na siyo kushambulia watu binafsi, kwani kufanya hivyo kunapunguza uzito wa hoja na kumfanya mdau wa mtandao kuonekana kama mchochezi badala ya mjenzi wa hoja.
Uzalendo wa kidijitali pia unadai kukataa katakata matumizi ya mitandao kupandikiza chuki za kidini, kikabila, au kisiasa zinazolenga kuwagawa Watanzania. Kauli zinazohamasisha watu kuasi mamlaka halali au kuingia mitaani kufanya vurugu, kama zile zinazojaribu kushawishi vijana wasishiriki katika sherehe za kitaifa au kususia shughuli za maendeleo, ni uchochezi unaopaswa kupingwa.
Amani ya nchi ndiyo inayowezesha mitandao hiyo kuwepo na kutumika; bila amani, hakuna jukwaa la kidijitali litakalokuwa salama. Ni wajibu wa kila kijana kutumia sauti yake mtandaoni kuzungumzia "Mazao ya Amani" kama vile fursa za kiuchumi, miradi ya kimkakati, na umoja wa kitaifa badala ya kugeuka chombo cha mabeberu na wachochezi.
Mwisho, vijana wanapaswa kutambua kuwa kila kitu wanachokiweka mtandaoni leo kinatengeneza historia yao ya kidijitali ambayo inaweza kuwasaidia au kuwaponza hapo baadaye.
Badala ya kutumia mitandao kama shimo la kulalamika na kutoa lawama zisizoisha, ni wakati wa kuitumia kama jukwaa la kibiashara, kuinadi miradi ya kijamii, na kutafuta fursa za kiuchumi zinazotangazwa na serikali kupitia wizara mbalimbali. Viongozi kama Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na wengine wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa vijana kuchangamkia fursa za mikopo na mitaji.
Kijana mjanja ni yule anayetumia simu yake kutengeneza andiko la mradi na kuliwakilisha kwa mamlaka husika, badala ya kutumia muda mwingi kusikiliza miradi ya vurugu ya watu wachache wenye nia ya kuivuruga Tanzania kwa maslahi yao binafsi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464