
Wakati Tanzania ikielekea kutimiza malengo yake ya Dira ya Maendeleo 2050, habari kutoka wilayani Kilwa mkoani Lindi zinatoa taswira mpya ya matumaini kwa vijana wanaotafuta mwelekeo wa kiuchumi.
Ziara ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko—ambao umefikia asilimia 90—ni kengele ya mwamko kwa kila kijana anayejitambua kuanza kujiandaa kuvuna matunda ya uchumi wa buluu.
Mradi huu mkubwa wa kimkakati, unaogharimu Shilingi bilioni 280, si tu ujenzi wa saruji na nondo, bali ni "kiwanda" cha ajira na biashara ambacho Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekidhamiria kama jawabu la kero za kiuchumi kwa Watanzania. Vijana wanapaswa kuelewa kuwa serikali imeshatengeneza mazingira; kazi iliyobaki ni kwao kuchangamkia fursa hizo kwa ubunifu na miradi madhubuti.
Maana ya Bandari ya Kilwa kwa Uchumi wa Kijana
Kukamilika kwa bandari hii kunafungua mnyororo wa thamani ambao haujawahi kushuhudiwa tangu uhuru. Kwa mujibu wa Meneja Mradi, Mhandisi George Kwandu, mradi huu utakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 1,800 za samaki kwa wakati mmoja na kuzalisha tani 100 za barafu kwa siku. Hii ina maana gani kwa kijana wa Kitanzania?
Kwanza, ni fursa ya viwanda vya uchakataji. Bandari hii itahitaji vifungashio, usafirishaji wa kisasa wa mazao ya bahari (logistics), na usambazaji. Vijana wanaweza kuanzisha kampuni ndogo za usafirishaji au ufungashaji zinazokidhi viwango vya kimataifa, kwani Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, amebainisha kuwa bandari hiyo inathibitishwa kwa viwango vya kikanda na kimataifa.
Pili, uamuzi wa Rais Dkt. Samia kununua meli tano za uvuvi za kisasa unamaanisha uhitaji wa wataalamu wa uvuvi, mafundi wa mitambo ya meli, na wasimamizi wa rasilimali za bahari. Hizi ni fursa ambazo kijana hawezi kuzipata kwa kukaa vijiweni au kulalamika mitandaoni; ni lazima kuanza kujifunza ujuzi husika na kutengeneza miradi ya kutoa huduma kwenye meli hizo.
Uchumi wa Buluu (Blue Economy) ni dhana pana inayohusisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji kwa ukuaji wa uchumi. Bandari ya Kilwa inakaribisha sekta binafsi kuwekeza kwenye mafuta ya boti, karakana za kutengeneza injini, na hata huduma za kijamii kama mahitaji ya chakula kwa wafanyakazi zaidi ya 30,000 wanaotarajiwa kunufaika katika mnyororo wa thamani
Kijana mwenye maono anaweza kuangalia fursa ya ujenzi wa maghala ya baridi (cold rooms) au biashara ya barafu kwa wavuvi wadogo wanaozunguka bandari hiyo. Hapa ndipo msisitizo wa Mzee Joseph Butiku unakuja—kwamba Rais ni nguzo yetu na anafanya kazi kwa ajili yetu sote. Miradi hii mikubwa inahitaji utulivu na amani ili iweze kuleta tija inayokusudiwa.
Wakati mradi huu ukikaribia kukamilika, vijana wanatakiwa "kujituliza" na kuelekeza nguvu zao kwenye maandalizi. Badala ya kushiriki kwenye mijadala ya uchochezi inayolenga kurudisha nyuma juhudi za serikali, huu ni wakati wa kuunda vikundi, kusajili kampuni, na kufuatilia taratibu za kisheria za kuwekeza Kilwa.
Dkt. Mwigulu Nchemba amewahakikishia Watanzania kuwa mradi huu utaacha alama. Alama hiyo itakuwa na maana zaidi ikiwa vijana wa Kitanzania ndio watakaokuwa mstari wa mbele kumiliki viwanda vya uchakataji samaki na kutoa huduma za kitaalamu bandarini hapo.
Ni wazi kuwa serikali ya awamu ya sita imeweka mezani mlo wa kutosha kupitia Uchumi wa Buluu. Kilwa imefunguka; meli tano zinakuja; ajira 30,000 zinatengenezwa. Swali pekee linalobaki kwa kijana mzalendo ni: Je, mradi wako upo tayari kuanza kuvuna dhahabu hii ya baharini? Amani na utulivu ndio mbolea pekee itakayofanya mbegu ya Bandari ya Kilwa kuota na kuneemesha maisha yako.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464