Katika kile kinachoonekana ni mkakati wa Serikali kusogea karibu na wananchi na kuzima chokochoko za uvunjifu wa amani, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, amefanya ziara ya kushtukiza mitaani na kwenye vijiwe vya vijana katika Halmashauri ya Mtama.
Ziara hiyo imekuja wakati ambapo Jeshi la Polisi Tanzania limetoa tamko rasmi likiwahakikishia Watanzania kuwa nchi ni shwari, licha ya kuwepo kwa juhudi za baadhi ya watu mitandaoni, akiwemo Maria Sarungi, wanaodaiwa kuchochea vurugu kwa kutumia picha za matukio ya zamani.
Mwanziva na "Diplomasia ya Vijiweni"
Akiwa wilayani humo, DC Mwanziva amekutana na makundi mbalimbali, ikiwemo vijana waendesha pikipiki (Bodaboda), ambapo amesikiliza kero zao na kutoa ufafanuzi wa fursa mbalimbali za kiserikali.
Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, limewataka wananchi kupuuza taarifa za uchochezi na kuendelea na shughuli zao za maendeleo. Polisi imesisitiza kuwa usalama umeimarishwa na hakuna dalili za vurugu kama zinavyopostiwa na baadhi ya watu walio nje ya nchi.
Taarifa ya Polisi imeeleza kuwa hali ya utulivu iliyopo ndiyo inayoruhusu viongozi kama DC Mwanziva kuendelea na ziara za kusikiliza kero za wananchi na kuhimiza ustawi wa jamii.
