Na Marco Maduhu, SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameshiriki kula chakula cha pamoja na watoto yatima pamoja na wanaoishi katika mazingira magumu, nyumbani kwake, ikiwa ni sehemu ya kuwapa faraja na kusherehekea nao Sikukuu ya Krismasi.
Amekula nao chakula hicho leo Desemba 25,2025, akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, pamoja na viongozi wa dini.
Amesema, inapofika siku za sikukuu, kila mtu huwa anamkimbilia mtu ambaye anamfahamu kwa ajili ya kumshika mkono kupata chochote kwenye sherehe hiyo, lakini amekuwa akijiuliza, watoto hao huwa wanamkimbilia nani, na hivyo kuamua kujitoa kwa kubeba jukumu hilo la kufurahi nao kwa kula chakula kila siku za sikukuu.
“Huwa najiuliza watoto hawa Malaika, ambao hawana wazazi na wengine kuachwa na kuishi mazingira magumu, huwa wanamkimbilia nani katika sherehe hizi za sikukuu, ili wafurahi kama watoto wengine ambao wanaishi na wazazi wao, nikaguswa na kuona ni vyema kuwapa furaha kwa kula nao chakula cha pamoja siku za sikukuu,”amesema Mhita.
Aidha, amesema haishii tu hapo kula nao chakula, bali ameomba apate orodha ya idadi ya watoto wote Yatima na ambao wanaishi katika Mazingira Magumu kutoka kwa walezi wa Vituo kwa kushirikiana pia na Maafisa Ustawi wa Jamii, ili awanunulie mahitaji yote ya shule , pamoja na kuwakatia Bima za Afya, ili wanapopata changamoto za kiafya watibiwe bure.
Ametoa pia salamu za upendo za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa mkoa huo, kwamba Rais anawatakia heri ya Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya 2026.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, amempongeza Mkuu huyo wa Mkoa, kwa upendo mkubwa aliouonyesha kwa watoto hao, na kwamba ametenda matendo ya huruma na Mungu ambariki, huku akitoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao kwa mujibu wa sheria na siyo kuwaacha wakiishi mazingira magumu huku mitaani.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo, naye amempongeza Mkuu huyo wa Mkoa, kwamba amefanya jambo la kiroho kwa kuthamini watoto hao, na kwamba Manispaa ya Shinyanga itaendelea kusaidia watoto hao kupitia Maafisa Ustawi wa jamii.
Kwa upande wao Mwakilishi wa baadhi ya Vituo vya kulea watoto hao Zainab Ramadhani kutoka kituo cha TAQWA kilichopo Bulugalila Kata ya Kizumbi, wamemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kula chakula pamoja na watoto hao, pamoja na kuahidi kuwanunulia mahitaji yote ya shule na kuwakatia Bima za Afya.
TAZAMA PICHA 👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita akizungumza.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akizungumza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga Salum Kitumbo akizungumza.
Mwakilishi wa kituo cha kulea watoto Zainab Ramadhani akizungumza.