` NDALA,MASEKELO ZATAJWA KINARA MATUKIO YA UHALIFU SHINYANGA

NDALA,MASEKELO ZATAJWA KINARA MATUKIO YA UHALIFU SHINYANGA


Na Marco Maduhu, SHINYANGA

JESHI la Polisi Wilaya ya Shinyanga limezitaja Kata za Ndala na Masekelo za Manispaa ya Shinyanga, kuwa zimekithiri kwa matukio ya uhalifu, ikilinganishwa na kata nyingine ndani ya manispaa hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 30, 2025 na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Shinyanga (OCD), Stephen Kimaro, wakati wa kikao cha ulinzi na usalama kilichowakutanisha viongozi wa serikali za mitaa, watendaji wa kata, Jeshi la Jadi Sungusungu pamoja na Polisi Kata, kilicholenga kuimarisha usalama wilayani humo.
Kimaro amesema kati ya kata 17 za Manispaa ya Shinyanga, Ndala na Masekelo ndizo zinazoongoza kwa matukio ya uhalifu, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa serikali za mitaa na Jeshi la Polisi ili kudhibiti vitendo hivyo.

“Kata za Ndala na Masekelo zimekithiri sana kwa matukio ya uhalifu tofauti na kata nyingine. Nawaomba viongozi wote tushirikiane kwa pamoja kukomesha vitendo hivi ili wananchi waendelee kuishi kwa amani na usalama,” amesema OCD Kimaro.
Aidha, amewataka pia viongozi wa serikali za mitaa pamoja na Jeshi la Jadi Sungusungu, kutoa taarifa za mapema kuhusu matukio ya kihalifu kwa Jeshi la Polisi, ili hatua za haraka zichukuliwe kabla madhara hayajatokea.

Kwa upande wake, Mratibu wa Polisi Jamii Wilaya ya Shinyanga Osward Nyorobi, amesema Manispaa ya Shinyanga kwa sasa inakabiliwa na wimbi la wizi wa taa za magari, hasa magari aina ya Subaru.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa, Sungusungu, kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi, kudhibiti pia vitendo vya uchomaji wa matairi barabarani wakati wa kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya, ili kuepusha uharibifu wa mali za umma na madhara kwa jamii.

Naye Kamanda wa Jeshi la Jadi Sungusungu Wilaya ya Shinyanga John Kadama, amesema jukumu la Sungusungu ni kulinda usalama wa wananchi, akisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na viongozi wa mitaa pamoja na Jeshi la Polisi, kuhakikisha uhalifu unakomeshwa na wananchi wanaishi kwa amani na utulivu.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Polisi wilaya ya Shinyanga OCD Stephen Kimaro akizungumza.
Mratibu wa Polisi Jamii wilaya ya Shinyanga Osward Nyorobi akizungumza.
Kamanda wa Sungusungu wilaya ya Shinyanga John Kadama akizungumza.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464