` DIWANI WA PUNI MHANDISI JUMANNE RAJABU AMUUNGA MKONO RAIS DK. SAMIA KUKUZA SEKTA YA MICHEZO

DIWANI WA PUNI MHANDISI JUMANNE RAJABU AMUUNGA MKONO RAIS DK. SAMIA KUKUZA SEKTA YA MICHEZO

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

DIWANI wa Puni Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Mhandisi Jumanne Rajabu, amemuunga mkono Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, katika suala zima kukuza sekta ya michezo, kwa kuimarisha miundombinu ya viwanja katika vijiji vyote vitatu vya Kata hiyo, ikiwamo kuweka magoli ya chuma, nyavu za kisasa, pamoja na kugawa mipira na jezi.
Mhandisi Rajabu, amebainisha hayo wakati akizungumza na vijana wa kijiji cha Buyubi, kwenye uwanja wa michezo wakati wakifanya mazoezi, kwa ajili ya kujiandaa na michezo wao wa kirafiki na timu nyingine kutoka kijiji jirani.

Amesema, michezo ina imarisha afya, kukuza vipaji vya vijana na hata kupata ajira kwa kusajiliwa kwenye timu kubwa, na ndiyo maana ameamua kukuza sekta ya michezo kwenye Kata hiyo, kwa kuimarisha miundombinu ya viwanja, pamoja na kufadhili ligi ambazo vijana wamekuwa wakicheza.
“Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan, anapenda sana michezo na amekuwa akiikuza sekta hiyo, na hata kutoa fedha kupitia goli la Mama kwa timu zinazoshiriki mashindano ya kitaifa, na mimi nimeona nisiwe nyuma nimuunge mkono Rais wangu, kwa kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo kwenye Kata yangu hapa Puni, ili vijana wakuze vipaji vyao na hata kusajiliwa kwenye timu kubwa,”amesema Mhandisi Rajabu.

Nao baadhi ya vijana hao, wamesema wanafariji kwa kuboreshewa miundombinu ya viwanja na kwamba awali walikuwa wakitumia magoli ya miti, huku wakicheza bila jezi na mipira mibovu, lakini sasa hivi wana goli za kisasa na nyavu zake, wana vaa jezi na wana mipira yote mipya.
Wamesema, vijana kushiriki michezo inawaepusha na matendo maovu ambayo hutokana na kukaa vijiweni, ikiwamo kuvuta bangi, kuwaza wanawake.

Wameeleza kuwa, kwa sasa vijana wengi baada ya kilimo, jioni hujumuika kwenye viwanja kwa ajili ya michezo, na kipindi cha kiangazi ndipo ligi huanza kuchezwa, na kumshukuru diwani wao kwa kwaunga mkono.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464