` DIWANI WA PUNI MHANDISI JUMANNE RAJABU AWAPONGEZA VIJANA WA BODABODA KUDUMISHA AMANI YA NCHI

WANDAMAN HOTEL

DIWANI WA PUNI MHANDISI JUMANNE RAJABU AWAPONGEZA VIJANA WA BODABODA KUDUMISHA AMANI YA NCHI

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

DIWANI wa Kata ya Puni, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Mhandisi Jumanne Rajabu, amewapongeza vijana wa bodaboda wa eneo la Njiapanda ya Didia kwa kuendelea kudumisha amani na kukataa kutumika vibaya na watu wachache wasioitakia mema Tanzania.

Rajabu ametoa pongezi hizo leo, Desemba 13, 2025, wakati akizungumza na vijana hao, akiwahimiza kuilinda amani ya nchi kwani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa wananchi.
Amesema endapo amani ya nchi itavurugika, shughuli za maendeleo zitasimama, hali itakayowaathiri zaidi vijana wanaojitegemea kwa kufanya kazi za kila siku, akiwamo waendesha bodaboda.

“Amani ya nchi ikivurugika, shughuli za maendeleo zitasimama na ninyi mtashindwa kujipatia kipato cha kuendesha maisha yenu na kuhudumia familia zenu, kwa sababu mtajikuta mkiwa ndani ya ‘lockdown’,” amesema Mhandisi Rajabu.
Anaendelea kusema anawashukuru vijana hao kwa msimamo wao wa kukataa kushiriki maandamano yasiyo na tija, akisisitiza kuwa amani ni tunu ya taifa inayopaswa kulindwa kwa wivu mkubwa.

“Nawashukuru sana vijana wa bodaboda kwa kuendelea kudumisha amani na kukataa kutumika kufanya maandamano yasiyo na afya. Amani ni tunu ya Taifa letu, hivyo tuilinde kwa wivu mkubwa na tumtetee Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, mama mwenye huruma na mwenye uchu na maendeleo ya wananchi,” amesema Mhandisi Rajabu.
Kwa upande wao, vijana wa bodaboda wakiongozwa na Paul Laurent wamesema hawapo tayari kutumika kuvuruga amani ya nchi, wakieleza kuwa wao ndiyo waathirika wakubwa pindi vurugu zinapotokea, kwani hushindwa kufanya shughuli za kujipatia kipato na familia zao kukosa mahitaji ya msingi.

Wamesema matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, na siku ya Uhuru, Desemba 9, kuambiwa kubaki majumbani, yamewaathiri pakubwa kutokana na maisha yao kutegemea kutoka nje kufanya kazi ili kupata ridhiki.

Naye James Lugembe, ameiomba serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kudumisha amani ya nchi, ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi bila hofu.

TAZAMA PICHA👇👇
Diwani wa Puni Jumanne Rajabu akizungumza na vijana njiapanda ya Didia juu ya kudumisha amani ya nchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464