
Hali ya amani na utulivu iliyoshuhudiwa jijini Dar es Salaam katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka wa 2025 ni kielelezo tosha cha utashi wa Watanzania kulinda mshikamano wa kitaifa dhidi ya mivutano ya kisiasa.
Maelfu ya wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya burudani wakisherehekea Krismasi na siku ya kupeana zawadi ya Boxing Day, huku kukiwa na mazingira ya usalama wa hali ya juu yaliyowezeshwa na uratibu makini wa vyombo vya dola.
Katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama Fukwe za Coco na kituo cha biashara cha Mlimani City, uwepo wa jeshi la polisi linalofanya doria kwa miguu, farasi, na magari umetoa uhakika wa usalama kwa kila familia iliyojitokeza kufurahia mapumziko hayo.
Utulivu huu una thamani ya kipekee ukizingatia kuwa unatokeo wakati kukiwa na jaribio la baadhi ya wanaharakati kuhamasisha maandamano katika kipindi hiki cha sikukuu, baada ya kushindwa kwa mipango yao ya awali ya maandamano haramu ya tarehe 9 Desemba, 2025.
Hata hivyo, Watanzania wameonyesha ukomavu mkubwa kwa kukataa shinikizo hizo na badala yake kuitikia wito wa kulinda amani, wakitambua kuwa ustawi wa uchumi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja unategemea utengamano wa nchi. Hatua hii ya wananchi kuipongeza serikali na polisi inaakisi imani kubwa ya umma katika usimamizi wa usalama unaoruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi kuendelea bila hofu.
Amani hii inayotawala mitaani inaenda sambamba na utulivu siyo tu inaimarisha furaha ya sikukuu, bali pia inatoa taswira chanya kwa wawekezaji na wadau wa biashara kuwa Tanzania inasalia kuwa kisiwa cha amani na mhimili wa uchumi wa kanda.
Uamuzi wa Watanzania kulinda amani kinyume na harakati za vurugu umesaidia kudumisha mazingira bora ya biashara na huduma, ambapo hakuna malalamiko yoyote ya uchelewaji au usumbufu yaliyoripotiwa katika kanda nzima ya biashara.
Hii inathibitisha kuwa nguvu ya umma imejielekeza katika kulinda mustakabali wa Taifa na ustawi wa kila mwananchi, ikizika rasmi ajenda za uchochezi na kuifanya Boxing Day ya mwaka 2025 kuwa alama ya amani ya kudumu nchini Tanzania.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464