Na Mwandishi Wetu
Kufuatia matukio ya kusikitisha yaliyotokea Oktoba 29, 2025, na siku zilizofuata, viongozi na wadau mbalimbali wameendelea kutoa wito kwa Watanzania kujikita katika uponyaji, maridhiano, na kujiamini katika mifumo ya ndani ya kutatua migogoro.
Katika sauti mbili tofauti zilizopatikana ikiwemo mtu anayejiita Mbunge wa Jimbo la Mtandaoni na ikitoka pia kwa Mtaalamu wa Sheria na Siasa wameeleza kiundani maana ya subira na uhuru wa nchi katika kukabiliana na changamoto zilizopo.
'MBUNGE'AOMBA KUKUNJUA MIOYO
'Mbunge' wa Jimbo la Mtandaoni, Bwana Gordon Kalulunga, ameharakisha kutoa wito wa dhati kwa Watanzania wenzake, akiwataka kusamehe na kusahau kufuatia matukio ya kusikitisha yaliyogusa kila mmoja nchini.
Akikiri kuwa si rahisi kwa mzazi kukiri, Bwana Kalulunga alikumbusha hatua za msingi zilizochukuliwa na uongozi wa nchi, ikiwemo Rais kusikitishwa, kuomba Bunge kusimama kuomboleza, na hata kutoa maelekezo ya kuwaondolea mashtaka watu waliokamatwa kuwa ni msingi wa uponyaji wa taifa.
"Natanguliza sentensi hiyo moyo wangu ukiwa unaukubali kwanza ukweli kabla sijawaomba watanzania wenzangu kukunjua mioyo. Ni jambo baya lilitokea. Yaliyotokea hayahitaji hotuba ndefu zaidi ya kuwaomba Watanzania tukunjue mioyo yetu na kuanza ukurasa mpya wa uponyaji maana maji yalishamwagika na hayazoleki," amesema Kalulunga katika mtandao wake.
Wito wake unasisistiza mazingira ya subira na kujiamini kwa Watanzania katika kutatua migogoro yao wenyewe.
TUME YA UCHUNGUZI
Kwa upande mwingine, mtaalamu wa Sheria na Siasa, Bwana Gulatone Masiga, ametetea kwa nguvu zote uamuzi wa Serikali wa kuteua Tume ya Uchunguzi yenye wajumbe wa ndani, akipinga hoja za wakosoaji wanaotaka wajumbe kutoka nje ya nchi.
Masiga anasisitiza kuwa uteuzi wa ndani unazingatia Uhuru wa Nchi na Mamlaka ya Katiba (Sovereignty), akionyesha kwamba Tanzania ina mifumo na wataalamu wenye uwezo wa kujichunguza na kujisahihisha bila kuingiliwa na taasisi za nje.
Tume si Hukumu, ni Uponyaji
Masiga anabainisha kuwa lengo kuu la Tume hii ni maridhiano ya kitaifa, sio hukumu ya kimataifa."Lengo la tume si kulipa kisasi au kutoa hukumu bali kuchambua tukio, kujifunza, kupendekeza marekebisho na kujenga maridhiano ya kudumu. Tume ya ndani ina uwezo mkubwa wa kuelewa mazingira ya kijamii, kisiasa, kisaikolojia na kitamaduni kuliko taasisi za nje," alisisitiza Masiga.
Aliongeza kuwa Mataifa yenye nguvu kama Marekani, Uingereza, na Afrika Kusini yanatumia Tume za ndani katika masuala nyeti, na hivyo Tanzania haikukosea.
Ulinzi wa Maslahi ya Kitaifa na Uzoefu Uliopo
Masiga alieleza wasiwasi wake kwamba kuingiza wajumbe wa kimataifa kunaweza kuhatarisha ulinzi wa Taarifa Nyeti na Usalama wa Taifa – Maslahi ya Kimkakati ya Taifa (Strategic National Interests).
"Tanzania tayari ina wanasheria, wanadiplomasia, na wataalamu waliothibitisha uwezo wao... Tunajivunia tume zilizofanikiwa kama vile Tume ya Jaji Nyalali (1991), Tume ya Maridhiano Zanzibar (2010), na Tume ya Rushwa (Warioba). Kwani kama hatuwaamini wataalamu wetu, tutawajengaje?" alihoji Masiga.
Masiga katika andiko lake alionya kuhusu historia ya taasisi za kimataifa, akisema baadhi yao zinaweza kuingia na ajenda zao za kisiasa, jambo ambalo linaweza kuleta migogoro mikubwa zaidi, akitoa mfano wa DR Congo na Libya.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464